Page 163 - EDK_F5
P. 163
SURA YA TANO KUFASIRI QUR’AN
Ngazi za tafsir ya Qur’an
Kazi ya 5 2
Shirikiana na wanafunzi wenzako, kusoma matini kuhusu ngazi za tafsir ya Qur’an,
kisha tofautisha baina ya tafsir Bil Maathur na Tafsir Bil Ray
FOR ONLINE READING ONLY
Kuna ngazi nyingi za Tafsir ya Qur’an, tokea ilipotambuliwa kuwa ni fani ya elimu
inayojitegemea karne ya tatu Hijriya hadi hivi sasa. Vimeandikwa vitabu vingi kuhusu
sayansi ya Qur’an, kwa kuwa Qur’an yenyewe imesheheni taaluma mbambali ndani yake.
Hata hivyo, kwa ujumla tafsir za Qur’an zinagawika katika ngazi mbili kubwa ambazo ni;
Tafsir Bil Maathur na Tafsir Bil Ray.
Tafsir Bil Maathur
Hii ni ngazi ya kwanza ya tafsir ya Qur’an, ambayo inazingatia ufafanuzi wa baadhi ya
aya za Qur’an kwa aya nyingine za Qur’an, ambazo zinabainisha zaidi kuhusu jambo
lililoelezwa katika aya za awali. Kadhalika, tafsir Bil Maathur inajumuisha ufafanuzi
wa Qur’an uliotolewa na Mtume Muhammad (S.A.W), kisha ufafanuzi uliotolewa na
maswahaba zake, kisha ufafanuzi uliotolewa na wanafunzi wa Maswahaba (Tabiin),
kuhusu aya katika Qur’an. Ni wazi kuwa hakuna yeyote anayeweza kuifasiri Qur’an
kama Allah (S.W) mwenyewe, Mtume wake (S.A.W), Maswahaba (R.A) na wanafunzi
wao (Tabi’in). Hivyo, ngazi hii ya tafsir inachukua daraja la kwanza.
Miongoni mwa kazi mashuhuri za tafsir Bil Maathur ni pamoja na; Jaamiul Bayan Fiy
Tafsirul Qur’an, iliyoandikwa na Imam Ibn Jarir Al-Twabari, aliyefariki mwaka 310H/
923 M. Bahrul Ulumi iliyoandikwa na Abu Layth Nasr ibn Muhammad Al-Samarkand,
aliyefariki mwaka 375 H. Al-Kashfu Wal-Bayan Tafsirul Qur’an, iliyoandikwa na Abu
Is’haq Ahmad ibn Tha’alab An-Naisaburi, aliyefariki mwaka 427 H. Tafsirul Qur’an
Al-Adhwiim, iliyoandikwa na Imam Ismail ibn Amr ibn Kathir, aliyefariki mwaka 774H
kama inavyoonekana katika kielelezo namba 5.3. Tafsir nyingine ni Ad-Durrul Manthur
Fiy Tafsir Bil Maathur iliyoandikwa na mwanazuoni Jalaluddin Suyutwi. Hizi ni baadhi
ingawa zipo nyingine, ambazo isingewezekana kuzitaja zote kwa sababu ya nafasi.
Kielelezo namba 5.3: Juzuu za Tafsiri ya Qur’an ya Ibn Kathir.
153