Page 166 - EDK_F5
P. 166
SURA YA TANO KUFASIRI QUR’AN
Mitizamo tofauti kuhusu tafsir Bil Ray
Kuna maoni tofauti kuhusu aina hii ya tafsir, wapo wanazuoni wanaopinga njia hii ya
tafsir, na wapo ambao wanaithibitisha. Wanaopinga njia hii wanatoa hoja kuwa, njia hiyo
ya tafsir inaongeza maneno katika maneno ya Allah (S.W) bila mamlaka. Kwa kuwa
hoja ya mfasiri wa rai itakuwa ni dhana pekee na hakuna uhakika kuwa hayo aliyosema
FOR ONLINE READING ONLY
ni makusudio halisi ya Allah (S.W). Kundi hili linaonesha kuhofia kutokana na Hadith
ya Ibn Abbas, kuwa Mtume amesema; Yeyote yule atakayetoa maoni yake binafsi katika
Qur’an ajiandalie makazi yake motoni.
Wanazuoni wa Tafsir Bil Ray, wanakanusha hoja hiyo ya wanaopinga kwa kusema kuwa,
ufafanuzi unaotolewa kwa kutegemea ijtihad stahiki, unatoa maarifa ya kutosha pale
ambapo hakuna nusus ya wazi iliyoeleza jambo hilo. Wanazuoni hao wanaifasiri Hadith
ya Ibn Abbas kuwa ilimaanisha; kufafanua au kusema kitu katika Qur’an bila ya ushahidi
au elimu au kwa utashi binafsi au ya kimadhehebu.
Wanazuoni wa Tafsir Bil Ray wanatetea pia kukubalika kwa njia hii ya Tafsir, kwa kauli
ya swahaba Abubakr (R.A), aliyesema kuwa; Nitatoa maoni yangu katika maneno ya
Allah (S.W), kama nitapatia basi itakuwa ni kwa sababu ya mwongozo wake, lakini kama
nitakosea basi ni makosa yangu mimi.
Kwa upande mwingine kukataza ijtihad katika kutafsiri Qur’an, kutafunga njia ya hukumu
nyingi za kisharia katika changamoto nyingi na zinazozidi kujitokeza. Kwa ujumla, tafsir
ya rai inayokatazwa ni ile inayofanywa kwa ujinga, uzushi na bila mazingatio.
Ukiangaliwa mtazamo wa wanazuoni wanaopinga Tafsir Bil Ray na simulizi za baadhi
ya Maswahaba na wanazuoni wakubwa wa kale, waliojiepusha na kufasiri Qur’an,
unagundua kwamba wote hao walijiepusha kwa sababu ya kiucha-Mungu, mashaka au
wasiwasi na hofu ya kukosea kwa kuwa hapakuwa na hali zinazohitaji jambo hilo.
Kwa hiyo, Tafsir Bil Ray zipo za aina mbili. Ya kwanza sio tu inakubalika bali inahitajika
na kusisitizwa, wakati nyingine sio tu inatakiwa kukatazwa bali ni haram. Tafsir Bil
Ray, inayokubalika ni ile inayotimiza vigezo, kama vile elimu stahiki, kuepukana na
chembechembe za ujinga, hadaa na upotoshaji.
Miongoni mwa Tafsir za rai mashuhuri na zinazokubalika ni pamoja na; Al-Tafsir al-Kabir
(Mafatih Al-Ghayb) iliyoandikwa na Imam Fakhruddin Al-Razi kama inavyoonekana
katika kielelezo namba 5.4. Imam Fakhruddin Al-Razi aliishi karne ya sita Hijriya
(544 hadi 606H), Tafsir Al-Baydhwawi, iliyoandikwa na Kadhi Abdullah ibn ‘Umar Al-
Baydhwawi, aliyeishi karne ya saba Hijriya na kufariki mwaka 691 H. Tafsir Jalalayn
156