Page 44 - EDK_F5
P. 44
SURA YA KWANZA ELIMU KATIKA UISLAMU
Ufupisho
Uislamu unaitazama elimu kuwa ni ujuzi ulioambatanishwa na utendaji. Aliyeelimika ni
yule aliyebadilika tabia na mwenendo wake kutoka katika hali duni kiutendaji, kuelekea
FOR ONLINE READING ONLY
hali ya ufanisi kutokana na ujuzi alioupata darasani au nje ya darasa, vitabuni au katika
mazingira yaliyomzunguka. Aliyesoma bila kutafsiri alichokisoma katika matendo ya
kila siku ni sawa tu na asiyesoma kwa sababu wote hawa hawainufaishi jamii.
Malengo ya elimu katika Uislamu ni kumuwezesha mja kumtambua Allah (S.W),
kuliendea na kulifikia lengo la kuumbwa kwake ambalo ni kumuabudu Allah (S.W).
Mja hawezi kumuabudu Allah (S.W) mpaka awe Khalifa. Yaani aweze kuiongoza jamii
kwa kufuata mwongozo wa Allah (S.W). Mfumo wa elimu wa Kiislamu ndio wenye
kumuwezesha mwanadamu kufikia malengo haya na kuikomboa jamii katika dimbwi
la ujinga na ujahili.
Elimu ya Kiislamu ni elimu inayojihusisha na fani zote za elimu, zinazosomwa kwa
kuzingatia lengo la elimu kwa mujibu wa Uislamu na kumtafakari Allah (S.W).
Mwalimu wa fani ya Qur’an, Tarekh, Fiqh, Akhlaq, Kemia, Biolojia na Fizikia,
anakuwa anafundisha elimu ya Kiislamu madhali anazingatia tafakuri juu ya Allah
(S.W).
Mgawanyo wa elimu ya dini na elimu ya dunia kama unavyopigiwa zumari na makafiri
na baadhi ya Waislamu, wasiojua makusudio halisi ya mgawanyo huo, haukubaliki
katika Uislamu. Mgawanyo huo husababisha Waislamu kutoipa kipaumbele elimu ya
mazingira, Wasomi Waislamu kutoipa thamani stahiki dini yao na Waislamu kushindwa
kuwa Makhalifa wa Allah (S.W) katika jamii.
Kwa kuwa kutafuta elimu ni faradhi kwa kila Muislamu, zama zote Waislamu wamekuwa
wakifanya juhudi za makusudi katika elimu, jambo ambalo limewafanya kubobea
na kugundua fani mbalimbali za elimu ikiwa ni pamoja na tiba, fizikia, unajimu na
kadhalika. Waislamu waliharibikiwa na kuwa duni kama hivi sasa pale walipokumbwa
na fitina ya Makafiri ya kutenganisha maisha ya dini na maisha ya dunia yaliyoambatana
na mgawanyo wa elimu katika tapo la dini na dunia.
Waislamu wanaweza kurudi katika hadhi yao ya juu katika jamii, endapo kila Muislamu
atajizatiti kusoma elimu ya mwongozo na mazingira kwa lengo la kumuabudu Allah
(S.W) katika kila kipengele cha maisha yake ya kibinafsi na kijamii na kwa lengo la
kusimamisha Ukhalifa katika jamii.
34