Page 9 - EDK_F5
P. 9
DIBAJI
Dibaji
itabu hiki cha somo la Elimu ya Dini ya Kiislamu kwa Kidato cha Tano ni katika
mfululizo wa vitabu viwili vya somo la Elimu ya Dini ya Kiislamu kwa shule za
Ksekondari Kidato cha Tano na Sita. Kitabu hiki kimetayarishwa kwa kuzingatia
FOR ONLINE READING ONLY
muhtasari wa mwaka 2024 na kina sura kumi zifuatazo:
1. Elimu katika Uislamu
2. Itikadi katika Uislamu
3. Nguzo za Imani
4. Ithibati ya Qur’an
5. Kufasiri Qur’an
6. Ithibati ya Sunnah
7. Utekelezaji wa nguzo za Uislamu
8. Uislamu na Mifumo ya Maisha
9. Historia katika Uislamu
10. Historia ya Uislamu
Sura hizo zimekidhi na kutosheleza umahiri mkuu, umahiri mahsusi na shughuli za
ujifunzaji kwa Kidato cha Tano kama ilivyo katika muhtasari.
Aidha, kitabu hiki kimetayarishwa kwa kuzingatia mbinu za kumuwezesha mwanafunzi
kujifunza kwa kutenda zaidi akiwa darasani na nje ya darasa. Hivyo, maudhui
yamewasilishwa kwa njia ya matini, kazi za kufanya na vielelezo ili kumvutia na
kumshajiisha mwanafunzi kukisoma. Pia, kitabu kina kazi na mazoezi ya kutosha ndani na
mwishoni mwa kila sura, ili kumuwezesha mwanafunzi aendelee kujipima na kujiimarisha
katika kukuza umahiri uliokusudiwa. Kwa hiyo, mwanafunzi anapaswa kufanya mazoezi
na kazi zote zilizomo ndani ya kitabu hiki, pamoja na kazi nyingine atakazopewa na
mwalimu zitakazomuandaa vema kufaulu mtihani wa Taifa.
Upekee wa Kitabu hiki ni kuwa maudhui na hoja zilizomo, zimetayarishwa kwa mtindo
mpya, licha ya kuwa huu ni mwendelezo wa ngazi ya Sekondari ya chini; Kidato cha
Kwanza hadi cha Nne. Kitabu hiki ni cha kiuchambuzi zaidi, ili kumwezesha mhitimu
kuwa mtendaji, mdadisi, mwenye upeo wa kutosha wa Elimu ya Dini ya Kiislamu na
mjengaji wa hoja. Hoja zimefafanuliwa kwa kiwango kinachoendana na Kidato cha Tano
na Sita ambapo baadhi ya hoja zimewekwa kwa makundi sio mojamoja kama ilivyokuwa
katika Sekondari ya chini. Mfano hoja zinazothibitisha kuwa Qur’an ni maneno ya Allah
(S.W) zimewekwa katika makundi manne.
vii