Page 107 - Historia_Maadili
P. 107

Ujenzi wa maadili

          Mapinduzi ya Zanzibar yalileta ukomo wa matabaka yaliyokuwapo kati ya Waarabu,
          Wahindi na Waafrika. Kwa kuondoa mfumo wa ubaguzi na ukandamizaji, Mapinduzi
          haya yaliweka misingi wa usawa wa kijamii, ambapo watu wote walihesabiwa kuwa
          na thamani sawa bila kujali asili yao. Hii ilijenga mazingira ya usawa, upendo, amani,
        FOR ONLINE READING ONLY
          heshima na mshikamano miongoni mwa watu wote. Serikali mpya ilisisitiza umuhimu
          wa demokrasia, haki za binadamu, utu, usawa na ustawi wa watu. Hii ilichangia katika
          kuhifadhi maadili ya jamii kama vile ushirikiano, usawa, kuheshimiana na kusaidiana
          ambayo ni sehemu muhimu ya utamaduni na utambulisho wa Mzanzibari.
          Sambamba na hayo, Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar yalichangia kukuza na
          kuendeleza lugha ya Kiswahili. Baada ya Mapinduzi, serikali mpya ilitilia mkazo
          umuhimu wa Kiswahili kama nyenzo muhimu ya kujenga umoja na utambulisho wa
          kitaifa. Kiswahili kikawa lugha rasmi ya serikali na wananchi wote wa Zanzibar.
          Ili kuhakikisha lugha hii inakua na kustawi, vilianzishwa vyombo mbalimbali vya
          habari kama vile magazeti ya Kiswahili, redio na baadaye vipindi vya televisheni.
          Pia, taasisi na wasomi walihimizwa kusoma na kuandika makala mbalimbali kwa
          kutumia lugha hii. Jambo hilo lilisababisha kuandikwa kwa kamusi na vitabu vya
          sarufi. Vitabu hivi vilikuwa nyenzo za elimu kwa lengo la kukuza Kiswahili katika
          maeneo mengine ya Afrika Mashariki na bara zima la Afrika.


          Serikali ilihamasisha matamasha mbalimbali ya kitamaduni ili kuimarisha umoja na
          mshikamano wa Wazanzibari. Kwa mfano, kuna matamasha kama Sauti za Busara,
          Sherehe za Mwaka Kogwa, Tamasha la Nchi za Jahazi Zanzibar (ZIFF), Tamasha
          la Vyakula vya Asili Makunduchi na mashindano ya mpira wa miguu ya Kombe la
          Mapinduzi. Haya matamasha yamesaidia na yanaendelea kusaidia, katika kuelimisha
          kizazi kipya kuhusu maadili, urithi wa kitamaduni na umuhimu wa kuuhifadhi.


                              Zoezi la          6.4


            1.  Bainisha  jitihada  zingine  zilizochukuliwa  na Serikali  ya Mapinduzi  ya
               Zanzibar katika kuujenga  umoja, usawa na mshikamano kwa jamii za
               Wazanzibari.


            2.  Eleza ni kwa namna gani lugha ya Kiswahili imefanikiwa kuwaunganisha
               Wazanzibari baada ya Mapinduzi.

            3.  Fafanua namna Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar  yanavyoenziwa  katika
               jamii ya sasa ya Watanzania.



                                                  99




                                                                                        03/10/2024   18:15:20
   HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd   99
   HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd   99                                         03/10/2024   18:15:20
   102   103   104   105   106   107   108   109   110   111   112