Page 103 - Historia_Maadili
P. 103
Hata hivyo, Waafrika ndio walioathirika zaidi katika mfumo wa kibaguzi wa kikoloni.
Pamoja na wingi wao kufikia 85% ya watu wote wakati wa Mapinduzi, walipata
huduma kidogo sana (chini ya 12%) ukilinganisha na wengine kama Waarabu na
Wahindi. Wahindi na Waarabu ndio waliopata nafasi kubwa zaidi katika kupata
huduma za kijamii, hasa maji, afya na elimu. Hivyo, ubaguzi katika nyanja mbalimbali
FOR ONLINE READING ONLY
ulileta chuki na kusababisha kuzuka kwa Mapinduzi ya Zanzibar mnamo Januari 1964.
Sababu za kiuchumi: Kabla ya ujio wa Waarabu, kilimo na uvuvi vilikuwa shughuli
kuu za kiuchumi kwa Wazanzibari. Wazanzibari walilima mazao ya chakula kama
vile mihogo, ndizi, nazi na mtama kwa ajili ya chakula na biashara. Pia, jamii
hizi zilijihusisha na shughuli za ufugaji na utengenezaji wa zana za kazi. Vilevile,
mazingira ya visiwa yaliruhusu uvuvi, ambao ulikuwa sehemu muhimu ya maisha
ya Wazanzibari. Jamii hizi zilitumia mitumbwi ya kienyeji, madema na nyavu za
mikono katika shughuli za uvuvi, hususani uvuvi wa samaki.
Hata hivyo, taratibu hizi zilibadilika mara baada ya kuja kwa wageni, yaani Waarabu
na baadaye Wazungu wakati wa ukoloni. Wageni, hususani Waarabu walinyakua
rasilimali kama vile ardhi nzuri kwa kilimo cha minazi na mikarafuu kwa manufaa yao
binafsi na ya ukoloni. Wazanzibari wengi walinyang’anywa ardhi yao yenye rutuba
na kubaki vibarua katika mashamba ya karafuu na minazi, pamoja na kufanya kazi
za ndani. Wahindi walitawala biashara zote za jumla na rejareja madukani wakiwa
pamoja na baadhi ya Waarabu. Hivyo, Mapinduzi ya mwaka 1964 yalikuwa ni ya
lazima ili kupinga na kuondoa utawala dhalimu wa kikoloni, kulinda rasilimali za
Wazanzibari na kujenga jamii inayozingatia misingi ya utu, usawa, haki na uwajibikaji
kiuchumi.
Chama cha ASP kilifanya mikutano ya hadhara na kutumia vyombo vya habari
kufichua maovu na unyanyasaji uliofanywa na wakoloni. Kwa mfano, mwezi
Desemba 1959, katika viwanja vya Raha Leo, Sheikh Abeid Amani Karume alitangaza
kwenye mkutano wa hadhara kwamba ASP ilitaka Zanzibar ipate uhuru na kuwa
jamhuri. Serikali ya kikoloni haikukubaliana na kauli hiyo. Kwa kuwa milango yote
ya kidemokrasia kwa Waafrika ilikuwa imefungwa, ASP iliona kuwa njia pekee ya
kuleta uhuru wa kweli Zanzibar ni mapinduzi. Ndipo ilipofika tarehe 12 Januari 1964,
ASP iliongoza Mapinduzi hayo na kuwakomboa Wazanzibari.
95
03/10/2024 18:15:19
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 95 03/10/2024 18:15:19
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 95

