Page 10 - Historia_Maadili
P. 10
Wakati huo huo, mataifa haya yalihitaji masoko mapya kwa bidhaa zilizozalishwa
na viwanda vyao na hivyo makoloni yalionekana kama masoko mapya ya bidhaa za
viwandani. Pia, mataifa haya yalihitaji maeneo ya kuwekeza mitaji yao ili kupata
faida kubwa. Hivyo, Bara la Afrika lilionekana kuwa suluhisho kwa uwekezaji huo
wa kibiashara. Kulikuwa pia na ushindani wa kisiasa na kijeshi kati ya mataifa ya
Ulaya Magharibi kutawala maeneo makubwa. Lengo lilikuwa ni kudhihirisha nguvu
FOR ONLINE READING ONLY
zao za kiuchumi na kijeshi na hasa kutawala sehemu muhimu za kimkakati. Sehemu
hizo ni kama vile njia za bahari za Atlantiki na Mediterania kupitia Bahari ya Shamu
hadi Bahari ya Hindi na mabonde muhimu kama Kongo, Naili, Niger na Zambezi.
Vilevile, kulikuwa na matamanio makubwa ya kueneza dini ya Kikristo, kwani
wamisionari waliona ni wajibu wao kueneza maadili ya Kikristo katika maeneo
mbalimbali, hasa barani Afrika. Wamisionari wa kwanza wa madhehebu ya Kikristo
katika jamii za Kitanzania walikuwa Ludwig Krapf na Johan Rebman. Katika
kupeleleza jamii za Kitanzania, wamisionari hawa walijifunza mila, desturi, maadili
na mazingira ya Kitanzania. Walijifunza pia fikra za wananchi na viongozi wa jadi,
ili kujua namna ya kuzitawala jamii hizo.
Ukoloni ulishamiri barani Afrika katika karne za 19 na 20. Wakoloni walitumia mbinu
mbalimbali kuanzisha na kuimarisha tawala zao. Mbinu hizo ni pamoja na mikataba
ya kilaghai, kutumia viongozi wa jadi ili angalau kupata ushawishi na hatimaye
kuzitawala jamii hizo. Moja ya mikataba ya kilaghai iliyosainiwa ni ule wa kati ya
Chifu Mangungo wa Usagara na Karl Peters, mwakilishi wa Wajerumani mwaka 1885.
Mkataba huo uliruhusu matumizi ya ardhi ya Usagara na uliweka msingi wa kukua
na kuenea kwa ukoloni wa Kijerumani katika maeneo yaliyoitwa Afrika Mashariki
ya Kijerumani.
Mikataba iliyosainiwa kati ya viongozi wa jadi na mawakala wa wakoloni ilikuwa na
masharti magumu na iliwanyima wenyeji haki ya kuihoji kabla ya kuisaini. Wakati
mwingine ukoloni ulikuwa na kuenea kwa kutumia nguvu za kijeshi. Maeneo ambayo
wenyeji walipinga uvamizi walishindwa kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo
ubora wa silaha za wakoloni ukilinganisha na silaha za jadi zilizotumiwa na jamii za
Kitanzania. Njia hii ya matumizi ya nguvu za kivita ndiyo iliyotumiwa zaidi kwani
jamii nyingi za Kitanzania hazikuwa tayari kuupoteza uhuru wao kirahisi.
Pia, wakoloni walitumia mbinu ya kuungana na baadhi ya jamii za Kitanzania dhidi
ya jamii nyingine. Hii ilitokea katika maeneo yaliyokuwa na uhasama kati ya jamii
za Kitanzania. Kwa mfano, Wajerumani waliungana na Chifu Merere wa Wasangu
na baadhi ya viongozi wa Wabena kuwapiga Wahehe waliokuwa chini ya utawala
wa Mtwa Mkwawa. Vilevile, Wajerumani waliungana na Mangi Mandara wa Moshi
kumpiga Mangi Sina wa Kibosho. Mara nyingi, wakoloni waliungana na jamii dhaifu
2
03/10/2024 18:15:05
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 2 03/10/2024 18:15:05
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 2

