Page 11 - Historia_Maadili
P. 11
ili kuzipiga jamii zenye nguvu na hivyo kujipenyeza na hatimaye kuimarisha tawala
zao.
Mkutano wa Berlin wa mwaka 1884 – 1885, pamoja na mambo mengine, ulilenga
kuligawanya bara la Afrika miongoni mwa mataifa ya Ulaya bila kujali mipaka
ya asili ya Waafrika na hivyo kuharakisha ukuaji wa tawala za kikoloni. Hii ilileta
FOR ONLINE READING ONLY
madhara makubwa kwa jamii za Kiafrika zilizokuwa zimejengwa katika misingi ya
utu, umoja, uzalendo na amani. Kukua na kuenea kwa ukoloni kulianza kusababisha
kuporomoka kwa maadili ya jamii nyingi za Kitanzania. Tamaduni nyingi za asili
zilianza kufifia kutokana na athari za ukoloni. Kwa mfano, lugha, mila na desturi za
asili zilianza kupotea au kubadilika kutokana na kuingiliwa, kudumazwa na kubezwa
na tamaduni za kikoloni.
Kazi ya kufanya 1.1
Umeteuliwa kuwa miongoni mwa wanafunzi watakaoshiriki mdahalo wenye mada
isemayo “Ukoloni ulikuwa na manufaa katika maadili ya jamii za Kitanzania.”
Soma vitabu na matini mbalimbali kisha andaa dondoo utakazozitumia wakati
wa mdahalo huo.
Mifumo ya kikoloni ya mataifa yaliyozitawala jamii za Kitanzania
Mifumo ya utawala ya Waarabu, Wajerumani na Waingereza katika jamii za Kitanzania
ilitofautiana kwa kiasi kikubwa, ingawa lengo kuu la mifumo hiyo lilikuwa kunyonya
na kupora rasilimali watu na rasilimali asilia za jamii za Kitanzania. Waarabu wa
mwanzo waliofika pwani ya Afrika Mashariki kabla ya karne ya 18, hawakuja kama
wakoloni bali kama wafanyabiashara. Hata hivyo, Waarabu kupitia utawala wa Sultani
wa Zanzibar kuanzia karne ya 18, walijikita zaidi katika biashara, hususani biashara
ya pembe za ndovu, watumwa, karafuu na nazi. Mfumo huu wa utawala ulitengeneza
tabaka la juu katika jamii, yaani tabaka la Waarabu na Wahindi waliojihusisha na
kilimo cha mashamba makubwa na biashara, huku Waafrika wengi wakibaki katika
hali duni ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Wajerumani walitawala jamii za Kitanzania kuanzia mwaka 1885 hadi 1919 baada ya
Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Katika utawala wao, Wajerumani walitumia mfumo
wa utawala wa moja kwa moja, uliokuwa na matumizi ya nguvu za kijeshi na sheria
kali dhidi ya watawaliwa. Jamii nyingi za Kitanzania ziliporwa ardhi na kulazimishwa
kufanya kazi katika mashamba na miradi ya kikoloni kama vile ujenzi wa reli na
miundombinu mingine kwa ujira mdogo. Wajerumani walitawala nyanja zote za
maisha ya Waafrika huku wakiendeleza miundombinu kwa ajili ya masilahi yao.
3
03/10/2024 18:15:06
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 3
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 3 03/10/2024 18:15:06

