Page 104 - Fasihi_Kisw_F5
P. 104

Fasihi ya Kiswahili  kwa Shule za Sekondari




                   (v)  Uaminifu ni hali ya mtu kuwa mnyoofu mwenye tabia njema
                        inayosababisha akubalike na watu na jamii inayomzunguka. Uaminifu
                        huzingatia  msimamo alionao mtu bila kuathiriwa  na ushawishi wa
                        mtu mwingine. Uaminifu hujenga imani na heshima. Pia, huimarisha
          FOR ONLINE READING ONLY
                        uhusiano mwema kuanzia ngazi ya familia na maeneo mengine kama
                        vile kazini,  kwenye nyumba za ibada, na kwenye asasi na taasisi
                        mbalimbali.

                   (vi)  Uwazi: unahusu fursa ya kila mwanajamii kujua mambo ya
                        kimaendeleo yanayotokea au kufanyika katika jamii yake. Uwazi
                        pia hutakiwa kudhihirishwa na kila mmoja kuanzia katika ngazi ya
                        familia.
              Umuhimu wa maadili katika jamii
              Maadili hujenga amani na utulivu na huleta umoja, ushirikiano na kuheshimiana
              miongoni  mwa  wanajamii. Hali  hii  huondoa  vitendo vya  ukatili  na  uonevu
              ambavyo huweza kusababisha migogoro au machafuko katika jamii.
              Zaidi ya kuleta maendeleo katika jamii, maadili huwafanya watu wawe wawazi,
              wakweli, na waaminifu katika kutunza mali au rasilimali za umma. Mathalani,
              viongozi  waadilifu  huweza kuchangia  maendeleo  kwa kusimamia  vizuri
              rasilimaliwatu na rasilimalifedha zilizoko katika maeneo yao ya kazi. Vilevile,
              maadili  hujenga  uzalendo  na  kufanya  kazi  kwa  bidii  kwa  ajili  ya  maendeleo
              binafsi na ya jamii kwa ujumla. Maadili huwafanya watu watambue umuhimu
              wa kushiriki katika miradi ya kijamii na kuchangia katika maendeleo ya sekta
              mbalimbali kama vile elimu na afya. Zaidi ya hayo, maadili hupunguza ufisadi,
              uhalifu na migogoro katika jamii. Kwa hiyo, maadili huchangia katika kuboresha
              maisha ya watu na kujenga ustawi. Umuhimu wa maadili umeweza kudhihirika
              katika  kazi  za  fasihi  kama  vile  bongo  fleva,  mashairi  na  tamthiliya  kama
              inavyofafanuliwa hapa chini:


              Maadili katika nyimbo za bongo fleva
              Nyimbo za bongo fleva zilianza kuimbwa kuanzia miaka ya 1990 hadi sasa na
              zimekuwa zikiimbwa na kupendwa sana na watu ndani na nje ya bara la Afrika.
              Nyimbo hizi  zimekuwa  zikiwavutia  watu kwa sababu mbalimbali  kama  vile
              mahadhi yake na matumizi ya lugha ya kisanaa. Baadhi ya nyimbo zimetumia
              lugha  ya  picha  katika  kufikisha  ujumbe  kwa  jamii.  Mbali  na  kutumia  lugha
              ya  kisanaa,  nyimbo  hizi  zimekuwa  zikielimisha  na  kuburudisha  kwa  namna
              mbalimbali.  Licha ya baadhi ya nyimbo hizi kukiuka misingi ya kimaadili
              kutokana na kutumia lugha zisizo na staha. Hata hivyo, nyingine zimekuwa
              zikizingatia maadili yanayofundisha na kujenga jamii.


                     Kitabu cha Mwanafunzi                                            93
                        Kidato cha Tano



                                                                                            23/06/2024   17:54
     FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd   93                    23/06/2024   17:54
     FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd   93
   99   100   101   102   103   104   105   106   107   108   109