Page 15 - Fasihi_Kisw_F5
P. 15
Fasihi ya Kiswahili kwa Shule za Sekondari
Wachambuzi wengine wenye mtazamo wa kidhanifu ni Felician Nkwera na John
Ramadhan. Katika insha yake kuhusu fasihi, Nkwera (1976) anasema “Fasihi ni
sanaa ambayo huanzia kwa Muumba, humfikia mtu katika vipengele mbalimbali...
(ni) hekima ambayo mtu ameshirikishwa apate kumtambua Muumba wake”.
FOR ONLINE READING ONLY
Akiunga mkono mtazamo huo, Ramadhan (1975) anasema kwamba, ingawa fasihi
ni hisi, kitendo cha mtu kuibuni kazi ya sanaa ni uigaji wa Mungu ambaye ndiye
mfalme wa sanaa zote. Mawazo ya wafuasi wa nadharia hii hayana uthibitisho
wowote zaidi ya kumtenga msanii na jamii yake kwa kumkweza na kuonekana
yuko karibu na Mungu kuliko wanajamii wengine. Aidha, wafuasi wa nadharia
hii wanaamini kuwa mwanafasihi hawezi kubuni kitu chochote zaidi ya kuiga
sanaa ambayo tayari Mungu ameitengeneza.
Nadharia ya kiyakinifu
Kwa mujibu wa Senkoro (1987), chimbuko la sanaa na fasihi ni mazingira
halisi ya jamii, hususani sanaa ya mwanzo iliyofungamana na kazi za uzalishaji
mali. Hii inamaanisha kwamba chanzo cha fasihi na sanaa ni binadamu (jamii)
na mazingira yake. Katika harakati za kukabili mazingira yake, ilimlazimu
binadamu kufanya kazi. Binadamu wa mwanzo aliishi katika mazingira yasiyo
rafiki. Hivyo, ilimlazimu kutumia silaha ili apambane na mazingira hayo. Huo
ndio ulikuwa mwanzo wa kutafuta njia za kurekebisha silaha zake (mawebutu)
kwa kuyachonga ili yawe na ncha kali. Uchongaji huo ndio ulikuwa sanaa
yenyewe. Kwa hiyo, hisia za kisanaa zimefungamana na maendeleo ya mtu
katika kupambana na mazingira yake na katika kufanya kazi. Nadharia hii ina
mwelekeo wa kukubalika zaidi, kwani inakubaliana na fikra kuwa wanadamu
walianza mawasiliano kupitia kazi zao. Kwa mantiki hiyo, chimbuko la sanaa ni
kazi.
Kadiri binadamu alivyozidi kuendelea, alikuwa na mahitaji mengine zaidi ya
mahitaji ya msingi. Mahitaji hayo yaliamsha hisia za kuchora vielelezo vya
shughuli zake za kujikimu. Michoro ya mapangoni iliyopo Kondoa (Tanzania) ni
mifano mizuri ya vielelezo hivyo. Kuzuka kwa lugha kuliongeza aina nyingine
ya sanaa ambayo ni fasihi.
Fasihi, kama zilivyo sanaa nyingine, ilitokana na kazi alizofanya binadamu
katika kupambana na mazingira yake. Fasihi ilianzia katika wimbo wa kazi.
Baadaye, tanzu nyingine za fasihi zilitungwa na kusimuliwa kwa madhumuni
ya kufunza, kukosoa, kuadibu, kuchokoza fikra na kuliwaza jamii baada ya kazi.
Kadiri maendeleo ya uzalishaji mali yalivyoongezeka, binadamu akapata muda
wa kupumzika na kustarehe kwa njia ya sanaa. Fasihi ilianza kutengana na kazi
4 Kitabu cha Mwanafunzi
Kidato cha Tano
23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 4 23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 4