Page 162 - Fasihi_Kisw_F5
P. 162
Fasihi ya Kiswahili kwa Shule za Sekondari
lugha, mtindo, na muundo unaotumiwa katika utanzu husika. Kufanya hivyo
humwongezea mtunzi maarifa ya namna ya kuandika kazi yake.
(f) Kuteua hadhira
Mwandishi huandika kazi yake ili iweze kusomwa na jamii. Kwa mantiki
FOR ONLINE READING ONLY
hiyo, hana budi kujua aina ya watu anaowaandikia kazi husika. Mwandishi
anatakiwa kujua mahitaji ya wasomaji wake, ikiwamo mitazamo yao kuhusu kile
anachokiandikia. Kwa mfano, kama mwandishi anawaandikia watoto, anatakiwa
kuandika kwa kutumia lugha nyepesi itakayowawezesha kuelewa maudhui hayo
kwa urahisi. Aidha, anaweza kuweka picha au michoro yenye rangi mbalimbali
ili kuwavutia watoto na kuwajengea kumbukumbu.
(g) Kuandaa zana
Katika hatua hii, mwandishi anaweza kubainisha vifaa na mahitaji mengine
ambayo yatamsaidia kuandaa kazi husika, zikiwamo shajara, kompyuta na simu.
Pia, mwandishi anaweza akaandaa ratiba ambayo itamwongoza katika mchakato
wote wa kuandika kazi yake kulingana na utanzu anaouandikia.
(h) Kuandika madondoo ya utunzi
Mwandishi anapaswa kuandika dondoo kuhusu sehemu muhimu za kazi yake.
Dondoo hizo, ambazo zitamwongoza katika uandishi wake, zinaweza kujumuisha
vipengele vya: majina ya wahusika wakuu, majina ya wahusika wengine,
mandhari, dhamira mbalimbali anazokusudia kuziwasilisha, mtindo wa uandishi
na mpangilio wa visa na matukio.
(i) Kuandika/kutunga
Baada ya kufanya maandalizi ya uandishi, mwandishi anapaswa kuanza
kuandika kazi yake kwa kuzingatia dondoo au mwongozo aliouandaa. Hapa
ndipo anapoweka mawazo yake katika maandishi kwa kuumba wahusika,
visa na matukio yanayosawiri wazo lake la ubunifu. Vilevile, katika hatua hii,
mwandishi hapaswi kuhofia makosa yoyote ya lugha bali aruhusu mtiririko wa
mawazo kwa mawanda mapana ili kukamilisha rasimu ya kwanza. Anatakiwa
kupangilia mawazo vizuri ili kuleta mantiki katika visa na matukio. Mawazo
au dhamira ndogondogo ni lazima zijengane na dhamira kuu. Aidha, mwandishi
aepuke kujaza mawazo ambayo hayana tija katika kazi yake. Hii inamaanisha
kwamba kila kinachoandikwa kiwe kinalenga kuiendeleza au kuikamilisha kazi.
Kadhalika, ahakikishe anawaumba vizuri wahusika ili kusawiri migogoro. Aidha,
atumie lugha ya kisanaa iliyojaa taswira, tamathali za usemi na mbinu nyingine
za kifasihi.
Kitabu cha Mwanafunzi 151
Kidato cha Tano
23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 151 23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 151