Page 163 - Fasihi_Kisw_F5
P. 163
Fasihi ya Kiswahili kwa Shule za Sekondari
(j) Kuboresha
Baada ya rasimu ya kwanza kukamilika, mtunzi anatakiwa kupitia au kukagua
kazi yake ili kufanya maboresho ya kiutungaji na kiubunifu. Mwandishi anaweza
kurekebisha mpangilio wa visa na matukio na kuongeza au kupunguza mambo
FOR ONLINE READING ONLY
yanayojirudia na yasiyokuwa na maana, au hata kubadilisha muundo wa sehemu
kadhaa za kazi yake. Vilevile, mtunzi anaweza kuwasuka upya wahusika ili
kuendana na mwelekeo wa usimulizi na matumizi ya lugha ili kuifanya kazi ivutie
na kuwa na kipekee. Pia, katika mchakato huu mwandishi anaweza kuboresha
miundo ya sentensi kwa kuondoa maelezo yasiyo ya lazima ili kuweka urahisi wa
kueleweka kwa wasomaji. Kwa hiyo, ni muhimu mwandishi kupitia kazi yake
mara baada ya uandishi ili kuhakikisha kazi ina mtiririko wenye mantiki, usahihi
wa taarifa, ushikamani wa kiusimulizi na ufikishaji wa ujumbe uliokusudiwa.
(k) Kuhariri
Hii ni hatua muhimu katika mchakato wa uandishi wa kazi za kifasihi. Katika hatua
hii, mwandishi anang’arisha na kuboresha maandishi ya kazi yake ili kuifanya
iwe sahihi na inayoeleweka kwa wasomaji. Hivyo, mtunzi hupaswa kuhariri kazi
yake kwa kuondoa makosa ya kiuandishi, kiuakifishaji na kimsamiati kama vile
sarufi, miundo ya sentensi na matumizi sahihi ya maneno. Vilevile, mwandishi
huweza kuhariri kazi yake kwa kuweka mtiririko mzuri wa uwasilishaji wa
matukio, mawazo na hisia ili kuifanya kazi ivutie zaidi. Mtunzi yupo huru kumpa
mtu mwingine ili ahariri kazi yake, hususani mtaalamu aliyebobea kwenye
utanzu husika na baadaye mhariri wa lugha. Hata hivyo, ingawa mchakato huu
ni muhimu ni vyema kuhakikisha kuwa uhariri hauharibu ubunifu na mtindo wa
lugha wa mwandishi.
(l) Kupitia kwa mara mwisho
Hii ni hatua ya mwisho katika uandishi, ambapo mwandishi huisoma upya kazi
yake ili kuchunguza na kurekebisha makosa madogomadogo kama vile tahajia
na sarufi. Lengo la usomaji huu ni kuhakikisha kazi inazingatia ubora, usahihi na
ufasaha. Baada ya hatua hii, kazi itakuwa imekamilika. Hivyo, inaweza kuendelea
na hatua za uchapishaji kutegemeana na malengo ya mwandishi.
Shughuli ya 6.6
Kwa kutumia vyanzo vya mtandaoni, maktabani au vinginevyo, jadili umuhimu
wa kufuata hatua za uandishi wa kazi ya fasihi.
152 Kitabu cha Mwanafunzi
Kidato cha Tano
23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 152
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 152 23/06/2024 17:54