Page 166 - Fasihi_Kisw_F5
P. 166
Fasihi ya Kiswahili kwa Shule za Sekondari
Shughuli 6.9
Tumia vyanzo vya mtandaoni, maktabani au vinginevyo, kueleza kanuni
zinazoongoza utunzi wa shairi.
FOR ONLINE READING ONLY
Kanuni za kutunga mashairi
Mashairi huwa na sifa za kipekee ambazo huyafanya kutofautiana na tanzu
nyingine za fasihi. Kwa mantiki hiyo, kuna mambo muhimu ambayo hayana budi
kuzingatiwa wakati wa utunzi wa mashairi. Mambo hayo ni lugha ya kishairi,
muundo, muwala, taswira na ishara, mtindo na utoshelevu.
(a) Lugha ya kishairi
Mashairi hutumia lugha ya mkato na kibunifu kama vile matumizi ya uwekevu,
tamathali za semi, misemo na nahau. Mwandishi anatakiwa kuzingatia vipengele
hivi ili kuleta mvuto wa shairi lake. Katika uandishi wa shairi, mtunzi ana uhuru
wa kukiuka kanuni za kisarufi ili kukidhi mahitaji ya ushairi.
(b) Muundo
Muundo wa mashairi unatofautiana na muundo wa matini nyingine za kifasihi
kwa sababu ya vipengele mbalimbali kama vile beti, mistari, mizani na miundo
mingine kulingana na aina ya shairi. Mwandishi hana budi kuandika shairi lenye
muundo unaosadifu mahitaji ya shairi lake; na kwa njia hii anaweza kuibua
muundo mpya tofauti na ile iliyozoeleka. Katika ushairi wa Kiswahili, miundo
iliyozoeleka ni ile ya kimapokeo na ya kisasa.
(c) Muwala
Mtunzi hana budi kuzingatia kipengele cha muwala ambacho hushughulikia
uwiano mzuri wa sehemu zote za shairi. Muwala huweza kupatikana kupitia
uzingatiaji wa mtiririko wa fikra katika umbo mahsusi la shairi ambao husaidia
kujenga mantiki ili kuwasilisha maudhui yaliyokusudiwa. Ushikamani wa kifikra
hutokea baina ya mshororo na mshororo, ubeti na ubeti, na hatimaye, shairi zima.
(d) Taswira na ishara
Mtunzi wa shairi haelezi mambo moja kwa moja bali huyafumbata anayotaka
kuyaeleza ndani ya taswira na picha zinazotumia ishara. Matumizi haya huathiri
hisia za wasomaji kama vile za upendo, huzuni, furaha, na hasira. Mbinu hii ya
matumizi mazuri ya lugha ya picha na ishara humfikirisha msomaji wa shairi kwa
kumfanya azifasili taswira na ishara hizo ili kupata maana iliyokusudiwa.
(e) Mtindo
Mshairi huwa na uwanja mpana wa kutumia mitindo mbalimbali kiuandishi.
Anaweza kutumia mtindo wa kimapokeo unaofuata kanuni za urari wa vina na
mizani au wa kisasa unaokiuka kaida na kanuni hizo.
Kitabu cha Mwanafunzi 155
Kidato cha Tano
23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 155 23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 155