Page 165 - Fasihi_Kisw_F5
P. 165
Fasihi ya Kiswahili kwa Shule za Sekondari
(a) Wazo au mgogoro
Igizo lolote, kama kazi yoyote ya sanaa, lazima liwe na wazo au mgogoro
unaovutia au wenye uzito. Mgogoro ni tatizo ambalo linahitaji utatuzi.
(b) Msuko wa matukio au matendo
FOR ONLINE READING ONLY
Hatua ya pili ya utunzi wa igizo ni uteuzi wa matukio yaliyopangiliwa katika
mfuatano wa usababishano – tukio moja likisababisha jingine, toka mwanzo
hadi mwisho. Msuko wa matukio unapaswa kuibua msisimko na taharuki kwa
wasikilizaji na watazamaji. Matukio haya huteuliwa na mtunzi lakini yanaweza
kubadilishwa katika uigizaji jukwaani.
(c) Matumizi ya dayalojia
Mazungumzo katika maigizo hayaandikwi, bali huibuka kulingana na
makubaliano baina ya waigizaji, na kufuata matukio yaliyopangwa.
(d) Wahusika
Wahusika katika maigizo wanatakiwa kuumbwa kwa kuzingatia mahitaji ya
vitendo husika. Wanatakiwa kuvutia, wawe wa kipekee na wauvae uhusika vizuri
ili kufanya uigizaji kuwa hai na kuhamasisha hisia kwa hadhira. Majukumu ya
wahusika yanatakiwa kuwa wazi na yanayoendana na dhamira ya igizo. Wahusika
kinzani huongeza msisimko na mvuto katika maigizo kwa sababu huchochea
migogoro, na migogoro ndiyo inayosukuma simulizi.
(e) Mandhari
Ijapokuwa mandhari ya igizo yanapaswa kuwa ya kuaminika na yenye uhalisi
ili kuendana na tukio, kuna maigizo yenye mandhari za kufikirika. Kwa jumla,
mandhari ya igizo inayovutia na iliyoundwa na mazingira ya kipekee, hufanya
simulizi ya igizo kuwa na nguvu ya ushawishi zaidi.
(f) Kugusa hisia za hadhira
Kazi ya maigizo ikisukwa vizuri huibua hisia na misisimko ya aina nyingine kwa
hadhira husika. Mwandishi anayegusa hisia za hadhira ndiye husemwa kuwa
kafanikiwa sana katika utunzi wake.
Ikumbukwe kuwa utunzi wa maigizo si wakuandika bali ni wa kuzungumza
na kutenda wazo kwa mujibu wa mfuatano mahususi wa matukio. Maigizo
hayasomwi bali husikilizwa na kutazamwa.
Shughuli ya 6.8
Chagua suala moja mtambuka, kisha tunga igizo kwa kuzingatia kanuni za utunzi.
154 Kitabu cha Mwanafunzi
Kidato cha Tano
23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 154
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 154 23/06/2024 17:54