Page 22 - Fasihi_Kisw_F5
P. 22
Fasihi ya Kiswahili kwa Shule za Sekondari
mtoto huyo kuwa kiongozi wao. Kiistiara, hadithi hii huweza kuwakilisha ukoloni
na mapambano ya kujikomboa. Zimwi linamwakilisha mkoloni, na mtoto ni
mkombozi. Pia, hadithi hii inaweza kuwa ishara ya kupigania haki ya aina yoyote
(Thomas, 2011)
FOR ONLINE READING ONLY
Kwa kawaida, ngano huwa fupi kwa sababu ya muundo wake wa kuwa na kisa
kimoja. Wahusika wa ngano ni bapa kwa maana kwamba mhusika akiwa mwema
ni mwema mwanzo hadi mwisho wa hadithi, vivyo hivyo kwa mhusika mwovu.
Lengo kuu la ngano, mbali na kuburudisha, ni kuadibu, kuadili na kuelimisha
jamii. Hujaribu kujenga utu bora kwa kueleza wema na ubaya.
(b) Tarihi
Tarihi ni hadithi zinazohusu matukio muhimu ya kihistoria. Msingi wa hadithi
hizi ni matukio ya kihistoria. Matukio haya yanaweza kuwa ya kweli au ya
kubuni au mchanganyiko wa ukweli na ubunifu. Aghalabu, wahusika wa hadithi
hizi ni binadamu. Miongoni mwa mifano maarufu ya tarihi ni Tarihi ya Kilwa.
Tazama mfano ufuatao:
Mji wa Kilwa na Watawala Wake
Hapo awali, Mji wa Kilwa ulikuwa ukitawaliwa na Waswahili wenyewe.
Kiongozi wa mwisho kabla ya ujio wa wageni alijulikana kwa jina la
Mndimbo. Alitawala mpaka karne ya saba. Watawala waliofuata walikuwa
wenye asili ya Kiarabu. Sultani wa kwanza, Ali bin-Hasan, alianza kutawala
mwaka 1200BK. Inasemekana alitengeneza sarafu ya kwanza. Utawala wake
ulifuatiwa na al-Hasan bin Daudi, ambaye alikuwa mjukuu wa Ali, lakini
wengine walipinga kwa kuwa alikuwa mpwa wake na utawala wake ulikoma
miaka ya 1300BK. Utawala mwingine ulianza mwaka 1300 ambapo al-Hasan
bin Talut alianza kutawala. Al-Hasan bin Talut alikuwa mtawala wa kwanza
katika ukoo wa tawala za Abu’ l-Mawahibu. Alikuwa na sarafu chache sana
zinazoashiria kipindi kifupi cha utawala wake. Mtoto wake aliyeanza kutawala
alijulikana kwa jina la Sultani Sulaiman bin al-Hasan. Isivyo bahati, mtawala
huyu haoneshwi katika orodha za Masultani katika fasili ya Kiarabu ingawa
kuna sarafu nyingi ambazo zinasemekana zilikuwa zake. Alishika madaraka
kwa miaka miwili tu. Mwaka 1320 al-Hasan bin Sulaiman alianza kutawala.
Mtawala huyu alitembelewa na Ibn Batuta mnamo mwaka 1331. Inasemekana,
huyu ndiye aliyejenga husuni kubwa na alikuwa na sarafu nyingi. Kuna habari
kuwa Mafia ilichukuliwa na Kilwa katika utawala huu. Mtawala aliyefuata
ni Daudi bin Sulaiman; huyu alikuwa ndugu wa al-Hasan bin Sulaiman.
Inasemekana alikuwa na sarafu chache sana na ndiye mtawala wa mwisho
kutengeneza sarafu kabla ya ujio wa Wareno (Massamba, 2017).
Kitabu cha Mwanafunzi 11
Kidato cha Tano
23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 11 23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 11