Page 25 - Fasihi_Kisw_F5
P. 25
Fasihi ya Kiswahili kwa Shule za Sekondari
(a) Methali
Methali ni semi za kimapokeo zenye hekima na busara zinazoelezea falsafa na
uzoefu wa jamii fulani kwa muhtasari. Semi hizi hubeba maana pana kuliko
maneno yenyewe yanayotumiwa. Methali hutumika kusisitiza, kuelimisha,
FOR ONLINE READING ONLY
kuonya au kupongeza kwa njia za busara. Aghalabu, methali hujengwa kwa
sitiari. Sitiari hizo hujitokeza katika pande mbili za methali ambazo hubainishwa
kwa mkato. Angalia mifano ifuatayo:
(i) Mtaka yote kwa pupa / hukosa yote.
(ii) Usipoziba ufa / utajenga ukuta.
(iii) Aisifuye mvua / imemnyea.
(iv) Chanda chema / huvikwa pete.
(v) Mtaka cha uvunguni / sharti ainame.
Mifano ya hapo juu inaonesha kuwa methali hubeba dhima mahususi. Kwa mfano,
methali (i) inawaasa wanajamii kutofanya mambo mengi kwa wakati mmoja. Ni
vyema kumakinikia jambo moja ili kulifanya kwa ufanisi, ndipo uanze jambo
jingine. Katika mfano wa (ii), jamii inaaswa kurekebisha tatizo katika hatua za
mwanzo, yaani kabla madhara makubwa hayajatokea.
(b) Misemo
Misemo ni tungo zitumiazo picha, ishara na tamathali kueleza kitu au wazo kwa
ufupi ili kuelimisha au kuadilisha. Misemo hufananisha maisha na matukio au
vitu. Wakati mwingine, misemo hutumika kutambulisha mazingira maalumu au
kuijulisha hadhira kuhusu hali fulani ya kijamii. Angalia mifano ifuatayo:
(i) Bendera hufuata upepo.
(ii) Elimu ni bahari.
(iii) Ukubwa jalala.
Mfano wa (i) unaonesha hali ya maisha, kwani wapo watu ambao hufuata mkumbo
bila kufikiria wala kuhoji kwa nini wanafanya jambo fulani na, hatimaye, kujikuta
kwenye matatizo. Katika mfano wa (ii), elimu inafananishwa na bahari. Bahari
ni kubwa, na haina mwisho, vivyo hivyo kwa elimu. Elimu hutupatia maarifa na
ujuzi wa aina mbalimbali. Pia, elimu haina ukomo, kwani binadamu hujifunza
kila siku. Mfano wa (iii) unalinganisha hali ya mtu kuwa mkubwa wa umri au
cheo, na kutupiwa lawama hata kama hajatenda kosa, kama lilivyo jalala ambapo
watu hutupa taka za aina mbalimbali.
14 Kitabu cha Mwanafunzi
Kidato cha Tano
23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 14
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 14 23/06/2024 17:54