Page 28 - Fasihi_Kisw_F5
P. 28
Fasihi ya Kiswahili kwa Shule za Sekondari
Ushairi simulizi hujipambanua na tanzu nyingine za fasihi simulizi kutokana na
matumizi ya mizani, lugha ya mkato, lugha ya mafumbo na uimbaji au ughani.
Mbali na kuzingatia mambo hayo yanayohusu ushairi kwa jumla, ushairi simulizi
una sifa ya kutungwa papo kwa papo na kufungamana na muktadha au tukio
FOR ONLINE READING ONLY
mahususi. Vipera vya ushairi simulizi ni nyimbo, mashairi, ngonjera, maghani
na tenzi. Wakati mwingine, mashairi huambatana na ala za muziki za jadi ama
za kisasa.
(a) Nyimbo
Nyimbo ni tungo za kishairi zinazowasilishwa kimuziki kwa kutumia sauti iliyo
katika mpangilio fulani wa mahadhi na melodia, na inayozingatia mapigo ya
kiurari. Mahadhi au tuni ni sauti mahususi ya uimbaji wa wimbo fulani, na melodia
ni mpangilio na mwendo wa uimbaji wenye kuzingatia urari wa mapigo au ridhimu
aghalabu hutofautiana kati ya jamii moja na nyingine. Nyimbo huweza kuimbwa
na kuchezwa pamoja na ala za muziki. Nyimbo huimbwa na mtu mmoja au kundi
la watu. Wakati mwingine, kikundi cha waimbaji huwa na kiongozi na wafuasi
wake. Kiongozi huanzisha wimbo, halafu wafuasi huitikia mkarara. Kiongozi
wa nyimbo huitwa manju. Nyimbo zinaainishwa kwa kuzingatia dhima, hadhira
inayoimbiwa na muktadha unaofungamana nazo. Kutokana na vigezo hivyo,
tunapata baadhi ya aina kama ifuatavyo: tumbuizo, bembezi, kongozi, nyimbo za
dini na wawe. Yafuatayo ni maelezo mafupi kuhusu aina hizi:
(i) Tumbuizo ni nyimbo za furaha ziimbwazo katika matukio mbalimbali
kama vile harusini na ngomani.
(ii) Bembezi/chombezi ni nyimbo za kubembelezea watoto.
(iii) Kongozi ni nyimbo za kuaga na kukaribisha mwaka.
(iv) Nyimbo za dini ni nyimbo zinazoimbwa kwa lengo la kumsifu Mungu
au miungu.
(v) Wawe ni nyimbo za kilimo zinazopatikana karibu katika makabila
yote ya Tanzania.
(vi) Mbolezi ni nyimbo zinazoimbwa kufuatia matukio ya huzuni, hasa ya
vifo.
(vii) Nyimbo za watoto ni nyimbo zenye maudhui mahususi kwa ajili ya
watoto.
Kitabu cha Mwanafunzi 17
Kidato cha Tano
23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 17 23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 17