Page 33 - Fasihi_Kisw_F5
P. 33
Fasihi ya Kiswahili kwa Shule za Sekondari
Wakati wa ukoloni, sanaa za jadi, hasa zile zilizohusiana na imani za dini,
zilipigwa vita. Hali hii ilisababisha sanaa kama vile matambiko kupotea katika
baadhi ya jamii. Sanaa nyingine zimedumu mpaka leo kutokana na wito wa
kitaifa wa kudumisha utamaduni wa Kitanzania na uimara wa jamii wa kutunza
FOR ONLINE READING ONLY
utamaduni wao.
Sanaa za maonesho mamboleo ni zile zilizotokana na athari za ujio wa wageni.
Sanaa za namna hii ni vichekesho na maigizo.
Majigambo
Majigambo ni masimulizi ya kujisifia au kujikweza kwa mtu kuhusu mambo
aliyowahi kufanya. Mambo hayo huwa ni ya kishujaa kama vile kupigana vita,
kuua wanyama wakali au kufanya jambo lolote kubwa la kishujaa. Kwa kawaida,
majigambo husimuliwa katika lugha ya kishairi na yanaweza kujitokeza katika
fasihi andishi na fasihi simulizi, zikiwamo bongo fleva na taarabu. Mjigambi
hufanya matendo mbalimbali. Aghalabu, mjigambi hubeba silaha kama vile
mkuki na ngao au upinde na mishale. Kama mjigambi ametoka kuua simba, kwa
mfano, ataonesha matendo ya jinsi alivyopambana na simba hadi kumshinda.
Makabila yenye sanaa za majigambo ni yale ya Ukanda wa Ziwa (kama vile
Wakurya, Wasukuma na Wahaya), yale ya Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania,
hususani Wahehe, na ya Kaskazini mwa Tanzania, hasa Wamasai. Majigambo
hufanyika wakati wa sherehe za harusi na za kuwapokea au kuwapongeza
mashujaa. Pia, hufanyika kwenye mikutano inayoitishwa na watawala. Majigambo
huambatana na ngoma na nyimbo za kusifu. Mjigambi hutokea katika kikundi
kinachocheza na kujigamba. Baada ya kumaliza, mjigambi mwingine hufuata.
Mara nyingi, mjigambi wa mwisho huwa yule aliyetenda jambo la kishujaa
kuliko wote au yule anayeijua vizuri sanaa ya majigambo.
Lengo kuu la majigambo ni kujenga ari ya ushujaa, ukakamavu na ujasiri. Mtu
anayefanya kitendo cha kishujaa, hushangiliwa na kupewa heshima kubwa katika
jamii yake. Kwa msingi huu, vijana huhamasika kuwa wajasiri na wakakamavu
ili kulinda hadhi na heshima ya jamii zao. Ijapokuwa, wajigambi wengi kwa
kawaida, huonekana kuwa wanaume hasa katika ngoma za kujigamba na kwenye
vikao vya pombe hata wanawake hujigamba katika miktadha tofauti ikiwamo ile
ambayo inawahusisha wanawake peke yao. Mfano mzuri ni katika taarabu, hasa
zile za mipasho. Kwa ujumla, majigambo hulenga kudumisha utu na heshima ya
mtu katika jamii.
22 Kitabu cha Mwanafunzi
Kidato cha Tano
23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 22 23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 22