Page 36 - Fasihi_Kisw_F5
P. 36
Fasihi ya Kiswahili kwa Shule za Sekondari
maingiliano ya muda mrefu. Makabila yote ya Mkoa wa Mara, kwa mfano, ni
watani wa Wanyaturu na Wanyiramba (Singida) na Wahaya (Kagera).
Utani hujenga uhusiano na ushirikiano mzuri baina ya wanajamii. Vilevile,
utani hutunza historia ya jamii zinazotaniana. Aidha, utani huwafunza watoto
FOR ONLINE READING ONLY
upendo na majukumu, mathalani, utani wa mjukuu wa kike na babu anapomwita
mke wake na kuomba amfanyie jukumu fulani, mtoto huyo hujifunza jukumu
lake atakalolitekeleza akiwa mkubwa. Vilevile, utani hukumbusha wanajamii
majukumu yao. Mathalani, katika misiba, watani hutumia tukio kukumbusha
watu kujuliana hali wanapokuwa wazima na kusaidia kazi zihusuzo msiba. Kama
zilivyo dhima nyingine za fasihi, utani huburudisha kwenye matukio ya furaha
na huzuni. Ikumbukwe kwamba, utani unaweza kusababisha ugomvi endapo
mhusika hajui kuwa anayemfanyia mzaha ni mtani wake.
(f) Maigizo
Maigizo ni sanaa inayotumia watendaji kuiga tabia na matendo ya watu au viumbe
wengine ili kuburudisha au kutoa ujumbe fulani. Maigizo haya yanapoletwa
jukwaani na kuoneshwa kwa hadhira huitwa drama. Mara nyingi, maigizo ya
Kiafrika huambatana na utambaji wa hadithi, vichekesho, nyimbo, matendo ya
kijadi kama vile harusi, jando na unyago. Wahusika hutakiwa kutumia lugha ya
kifasihi inayoendana na hadhira. Zipo aina mbalimbali za maigizo, zikiwamo
maigizo ya misibani na mivigani, maigizo ya watoto na ya burudani.
(g) Michezo ya watoto
Watoto hucheza michezo mingi yenye kuambatana na usanii. Michezo hiyo
hutofautiana majina kulingana na mahali. Katika michezo hiyo, kuna kuimba,
kucheza, kurukaruka, kukimbia, kughani, kujigamba na kuigiza. Baadhi ya
michezo hiyo ni: kiota, ukuti, pembea (bembea), kitikiti, kibuzi na kombolela.
Aghalabu, michezo hiyo huambatana na nyimbo, majibizano, vitendo na maigizo.
Kwa mfano, katika mchezo wa kiota, watoto hunyanyuka pale walipoketi na
kuanza kutangatanga huku na huku ilihali wakiimba mpaka kila mmoja anapopata
mahali pake na kukaa. Watoto huimba hivi:
Kiota
Sisi ndege twaruka
Twatafuta kiota
Kiota
Kiota
Kiota
Kitabu cha Mwanafunzi 25
Kidato cha Tano
23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 25 23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 25