Page 40 - Fasihi_Kisw_F5
P. 40
Fasihi ya Kiswahili kwa Shule za Sekondari
kueleza maudhui yake kimuhtasari; na aghalabu, huyaficha maudhui hayo ndani
ya taswira na ishara. Kama ilivyo kwa ushairi simulizi kwamba ndio utanzu wa
kwanza kabisa wa fasihi simulizi, ushairi andishi nao ulikuwa utanzu wa kwanza
wa fasihi andishi.
FOR ONLINE READING ONLY
Historia fupi ya ushairi wa Kiswahili
Tarehe mahususi za kuanza kwa ushairi wa Kiswahili, hususani umbo la ushairi
linaloonekana leo, ni za kukisia. Kilicho bayana ni kwamba, kabla ya karne
ya 10 ushairi wa Waswahili ulikuwa ukitungwa na kughaniwa kwa ghibu bila
kuandikwa. Hali ilibadilika kuanzia karne ya 10 wakati Uislamu ulipoanza
kuenea Uswahilini; na hivyo, kueneza hati ya Kiarabu. Kuanzia wakati huo,
baadhi ya Waswahili walianza kutunga na kuandika mashairi, hasa tenzi na tendi,
kwa kutumia hati hiyo.
Wataalamu hugawa maendeleo ya ushairi wa Kiswahili katika mihula mbalimbali.
Kwa mfano, Kezilahabi (1983) anabainisha mihula minne ambayo ni: muhula wa
urasimi, muhula wa utasa, muhula wa urasimi mpya, na muhula wa sasa.
Muhula wa Urasimi ni kipindi maalumu kinachochukuliwa kuwa msingi wa
kuwekwa kwa sheria au kanuni ya jambo fulani. Urasimi wa ushairi wa Kiswahili
ulipata mashiko katika karne ya kumi na nane (1700-1800). Katika kipindi hicho,
kulikuwa na tungo kama vile Utenzi wa Hamziyya (bin Uthman, 1690), Utenzi
wa Tambuka (Bwana Mwengo, 1728), Utenzi wa Al-Inkishafi (bin Nasir, 1800)
na Utenzi wa Mwanakupona (Mwanakupona bint Mshamu, 1858). Tungo hizi
zilitanguliwa na tungo zilizohusu simulizi za Fumo Liyongo na zikafuatiwa
na tungo za Muyaka bin Haji. Baada ya hapo, ulifuatia ukame wa tungo kwa
kipindi cha takribani miongo mitano (1885 - 1945). Kulikuwa na tungo chache;
ndiyo maana muhula wa pili unaitwa muhula wa utasa. Sababu za ukame huu ni
pamoja na matukio ya vita yaliyotokea ulimwenguni. Baada ya hapo, ukafuatia
muhula wa urasimi mpya ambapo kulikuwa na watunzi kama vile Shaaban
Robert, Kaluta Amri Abedi na Mathias Mnyampala. Huu ni muhula ulioshuhudia
kuimarishwa kwa kanuni za utungaji wa ushairi wa Kiswahili kama vile Sheria
za Kutunga Mashairi na Diwani ya Amri (Abedi, 1954). Kisha, ulifuatia muhula
wa sasa. Muhula huu ulianza wakati mataifa ya Afrika Mashariki yalipopata
uhuru kutoka kwa wakoloni. Hiki ni kipindi kilichokuwa na wasomi wengi wa
ngazi ya chuo kikuu waliojihusisha na utungaji, uhakiki na utafiti kuhusu masuala
ya fasihi, ukiwamo ushairi. Hali hii mpya ilisababisha kuwapo kwa fikra mpya
katika ushairi wa Kiswahili; ndipo ulipoibuka mjadala kuhusu ushairi usiofuata
urari wa vina na mizani. Mjadala huo hujulikana kama Mgogoro wa Ushairi
ambao umeelezwa kwa urefu katika kitabu cha Mulokozi na Kahigi (1982).
Kitabu cha Mwanafunzi 29
Kidato cha Tano
23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 29 23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 29