Page 42 - Fasihi_Kisw_F5
P. 42
Fasihi ya Kiswahili kwa Shule za Sekondari
Shairi hili lina mizani linganifu. Kila mshororo una mizani kumi na sita na vina
vinavyofanana mwishoni mwa kila mshororo kwa shairi zima. Vina vya kati
vinafanana katika kila ubeti. Kila ubeti umeundwa na mistari minne, ambapo
huu ni muundo wa tarbia.
FOR ONLINE READING ONLY
Mtazamo wa kisasa au masivina
Huu ni mtazamo wa wanamabadiliko wanaodai kwamba si lazima shairi liwe
na urari wa vina wala ulinganifu wa mizani. Mtazamo huu ulianza mwishoni
mwa miaka ya 1960 na kushadidiwa mwanzoni mwa miaka ya 1970. Wafuasi wa
mtazamo huu ni Ebrahim Hussein, Euphrase Kezilahabi na Jared Angira. Wafuasi
wengine ni Mugyabuso Mulokozi, Kulikoyela Kahigi, Said Ahmed Mohamed
na Theobald Mvungi. Kulikoyela Kahigi na Mugyabuso Mulokozi wameandika
Mashairi ya Kisasa (1973), Malenga wa Bara (1976) na Kunga za Ushairi na
Diwani Yetu (1982), Said Ahmed Mohamed ameandika diwani kadhaa zikiwamo
‘Sikate Tamaa (1983) na Kina cha Maisha (1984).
Wafuasi wa mtazamo huu wanaamini kuwa maudhui yanaweza kuwasilishwa
bila kujikita katika sheria za vina na mizani. Wanadai kuwa, kama ambavyo
mabadiliko yanatokea katika nyanja nyingine, ni lazima pia yatokee katika
ushairi. Ikumbukwe kwamba, wenye mtazamo huu hawapingi kanuni za
wanamapokeo, ila wamepanua wigo wa mashairi. Kwa mfano, zaidi ya nusu ya
mashairi yaliyomo katika Diwani ya Malenga wa Bara (Kahigi na Mulokozi,
1976) ni ya kimapokeo. Wanausasa wanatilia mkazo matumizi ya lugha kuliko
muundo wa shairi. Tazama mfano wa shairi la kisasa la “Kuchambua Mchele”:
Habari zilifika kutoka Arusha,
Tukaanza kuchambua mchele wa Ujamaa,
Macho mbele, macho pembeni tukitoa mchanga,
Tukafanya kaburi dogo la mchanga.
Tukaanza kutoa chenga, moja moja,
Vidole vikafanya kazi kama cherehani,
Usiku na mchana; macho yakauma,
Tukafanya kichuguu kidogo cheupe.
Kichomi (Kezilahabi, 1988)
Kitabu cha Mwanafunzi 31
Kidato cha Tano
23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 31 23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 31