Page 32 - Fasihi_Kisw_F5
P. 32
Fasihi ya Kiswahili kwa Shule za Sekondari
Beti hizi ni sehemu ya simulizi ya kiutendi inayomhusu Fumo Liyongo. Simulizi
hii inaakisi maudhui ya kipindi cha miaka ya 900-1500 BK. Hivyo, lugha
iliyotumika ni ile inayoakisi kipindi hicho. Pia, simulizi katika utendi huu inahusu
masuala kama vile nguvu za kimwili, kiakili, kisihiri, kivita na kiume (urijali).
FOR ONLINE READING ONLY
Shughuli ya 2.5
(a) Tunga kazi kwa kutumia kipera kimojawapo cha ushairi.
(b) Chagua suala mtambuka mojawapo katika jamii kisha andaa majigambo.
Shughuli ya 2.6
Jadili sanaa za maonesho kwa kuzingatia maana, aina na sifa zake.
Sanaa za maonesho
Balisidya na Muhando (1976) wanadai kwamba sanaa za maonesho ni sanaa
ambazo huwasilisha wazo ana kwa ana kwa kutumia usanii wa utendaji. Utanzu
huu hujumuisha kipera chochote chenye mambo yafuatayo:
(i) Dhana ya kutendeka (tendo);
(ii) Mtendaji (fanani);
(iii) Uwanja wa kutendea (jukwaa);
(iv) Watazamaji (hadhira); na
(v) Kusudio la kisanaa (maudhui).
Sanaa za maonesho huwa kwenye umbo linalotendeka. Huweza kugawanyika
katika makundi mawili ambayo ni sanaa za maonesho za jadi na sanaa za
maonesho mamboleo. Sanaa za maonesho za jadi ni zile zilizochipuka katika
jamii za Kiafrika. Sanaa hizi hujumuisha majigambo, miviga, vichekesho,
ngomezi, tambiko, utani, maigizo na michezo ya watoto. Ingawa miviga kama
vile ibada, sherehe, jando na unyago ni matukio ya kijamii au kimila yenye
kuvuka mipaka ya kisanaa, lakini inajumuishwa hapa kwa kuwa sanaa hutawala
utendaji na uwasilishaji wa maudhui yake. Wakati wa uwasilishaji wa shughuli
hizi, watu hufanya vitendo vya kisanaa kama vile uigizaji wa visasili, uchezaji
ngoma, uimbaji na utongoaji mashairi, vikiambatana na matendo ya mwili. Kwa
njia hii, watu huweza kuwasiliana wao kwa wao au kuwasiliana na miungu.
Ijapokuwa dhima ya sanaa hizi hufanana kwa namna ya jumla, huwa kuna tofauti
mahususi katika vipengele vya utendaji kati ya jamii au kabila moja na jingine.
Kitabu cha Mwanafunzi 21
Kidato cha Tano
23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 21 23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 21