Page 34 - Fasihi_Kisw_F5
P. 34

Fasihi ya Kiswahili  kwa Shule za Sekondari




              (a)  Matambiko
              Matambiko ni ibada zinazoambatana na utoaji wa sadaka kwa Mungu, miungu na
              mizimu. Tangu zamani, jamii mbalimbali zilifanya matambiko ili kutoa shukrani,
              kusifu, kuomba msamaha na kadhalika. Tambiko ni tukio halisi ambalo baadhi
              ya matini  zinazotumika  huwa na maneno ya kisanaa. Licha ya matumizi  ya
          FOR ONLINE READING ONLY
              lugha ya kisanaa kama vile tamathali za semi, taswira na lugha ya mafumbo
              kwa ujumla, matini za ushairi wakati mwingine husheheni nduni za ushairi ndiyo
              maana linaingizwa katika kundi la sanaa za maonesho. Kwa kawaida, matambiko
              hufanywa na watu maalumu katika jamii. Matambiko hufanyika katika maeneo
              maalumu. Kwa mfano, watambikaji katika baadhi ya jamii za Kanda ya Ziwa
              huelekeza  maombi  yao  kwa  Namhanga  (Mungu Mkuu),  Mugasa  (mungu  wa
              wavuvi) au Kalungu (mungu wa wawindaji). Utendaji wa tambiko hili huenda
              sanjari na matumizi ya maleba, vyungu na pembe maalumu. Sadaka zitolewazo
              na jamii ya Wakerewe hujumuisha kuku, mbuzi, kondoo, ng’ombe, vyakula vya
              nafaka na pombe huitwa empahe.

              (b)  Miviga
              Miviga ni sherehe au shughuli zinazofanywa na jamii katika kipindi maalumu
              cha mwaka au katika muktadha maalumu. Sherehe hizo zinaweza kuwa za jando
              na unyago, harusi, au kutawazwa kwa Mtemi. Miviga ni sherehe zihusuzo mtu
              kutoka katika  kundi au wadhifa fulani  na kuingia  katika  wadhifa mwingine.
              Mathalani, anaweza kutoka katika rika la utoto kwenda ujana (jando na unyago)
              na ujana kwenda utu uzima (kuoa au kuolewa). Kadhalika, miviga ni matendo ya
              kimila ambayo wakati mwingine huhusisha sehemu kubwa ya jamii.

              Miviga huambatana na maigizo na nyimbo zinazoendana na tukio husika. Katika
              harusi, nyimbo zinazoimbwa ni za ndoa; na katika mazishi nyimbo zinazoimbwa
              ni za maombolezo.  Katika miviga, ngoma mbalimbali huchezwa.  Aghalabu,
              wazee hutoa mafunzo na mawaidha, hususani kwa watoto na vijana.

              (c)  Vichekesho
              Vichekesho ni aina ya sanaa ya fasihi simulizi. Katika sanaa hii, watu husimulia
              visa na mikasa ambavyo huwafanya wasikilizaji  na watazamaji  wacheke.
              Vichekesho vinahitaji ubunifu mkubwa ili kupata jambo litakaloibua hisia na
              kuvunja  mbavu.  Lugha inayotumika  katika  vichekesho  ni nyepesi  na iliyojaa
              picha  ambazo watazamaji wana uwezo wa kuzitambua. Hii ni kwa sababu
              hutumia mifano ya vitu vinavyojulikana wazi kwa hadhira au vinavyopatikana
              katika mazingira yao. Aidha, vichekesho hutumia mbinu ya kejeli, dhihaka na
              utani.






                     Kitabu cha Mwanafunzi                                            23
                        Kidato cha Tano



                                                                                            23/06/2024   17:54
     FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd   23                    23/06/2024   17:54
     FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd   23
   29   30   31   32   33   34   35   36   37   38   39