Page 23 - Fasihi_Kisw_F5
P. 23
Fasihi ya Kiswahili kwa Shule za Sekondari
(c) Visasili
Visasili ni hadithi zinazoelezea chimbuko au asili ya jamii, ukoo, au kundi fulani.
Huelezea pia tamaduni mbalimbali na namna jamii fulani ilivyofika katika eneo
fulani. Kadhalika, visasili huelezea na kufafanua masuala ya kimaumbile na
FOR ONLINE READING ONLY
kiimani yanayomhusu na kumsumbua binadamu kama vile maradhi na kifo.
Visasili hueleza pia maana ya maisha na hatima ya mwanadamu kulingana na
imani za jamii inayohusika. Kwa kawaida, visasili huheshimiwa na kuaminiwa
na wanadamu, na huhusishwa na kuwa vielelezo vya miviga na ibada zao. Mfano
wa kisasili ni hadithi za mataifa mbalimbali kuhusu kuumbwa kwa ulimwengu
na vilivyomo. Mfano mzuri ni hadithi ya Wakikuyu ya “Gikuyu na Mumbi”
ambayo inapatikana katika kitabu cha Naushangilia Mlima Kenya (Kenyatta,
1966), simulizi ya “Asili ya jina la Wakinga” kutoka kwa Wakinga, na simulizi ya
“Adamu na Hawa” kutoka Mashariki ya Kati ambayo inapatikana katika Biblia
na Kurani.
Mfano wa Kisasili
Asili ya Jina la Wakinga
Wenyeji wa jamii ya Wakinga wanapatikana Nyanda za Juu Kusini katika
eneo lenye vilima, uoto mzuri wa asili na vijito vinavyotiririka kama mkufu
usio na mwisho. Wenyeji wa jamii hii walikuwa na shughuli mbalimbali tangu
enzi za zamani. Walijishughulisha na ufuaji chuma, viazi, ngano na njegere.
Palipo na ustawi hapakosekani adui. Jamii hii ilikuwa na mbinu zake za siri
za ulinzi ambazo kila mwanajamii alifundishwa katika makuzi yake. Wakinga
walikuwa na maadui na walipigana vita mara kwa mara na kuvishinda vita
hivyo. Adui alipovamia ardhi ya Wakinga, kiongozi alijitokeza na kupiga
kelele ‘Vakinga Vakinga!’ (maana yake jihadhari) akiwa amepanda juu ya
kilima. Baada ya hapo kila mwanajamii alitambua kuwa hiyo ni vita na kila
mmoja aliwajibika kupambana. Wazee waliongoza jamii nzima kwa kutoa
ushauri na kuombea ushindi, vijana walichukua silaha za kivita, wanawake
na watoto walikimbilia kwenye mahandaki. Huo ndio mwanzo wa Wakinga
kuitwa Wakinga kulikotokana na sauti hiyo ya tahadhari.
(d) Vigano
Vigano ni hadithi fupifupi za kifasihi simulizi. Mafunzo yake hutolewa kwa
kutumia lugha ya picha kama ilivyo kwa methali. Hadithi hizi zina hadhi ya
methali ingawa hutumia taswira pana kuliko methali. Kimsingi, hadithi za namna
hii hutolewa kama vielelezo, hasa wakati wa mazungumzo au maongezi. Lengo
kuu huwa ni kumkanya na kumfunza anayesikiliza.
12 Kitabu cha Mwanafunzi
Kidato cha Tano
23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 12
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 12 23/06/2024 17:54