Page 53 - Fasihi_Kisw_F5
P. 53
Fasihi ya Kiswahili kwa Shule za Sekondari
(a) Tanzia
Tanzia ni tamthiliya zenye tukio au matukio ya kuhuzunisha; nayo huhusika na
mambo yenye uzito kifikra na kihisia, katika maisha ya binadamu. Mhusika mkuu
ambaye kwa kawaida ni mtu maarufu mwenye kupewa sifa nyingi zinazovutia,
FOR ONLINE READING ONLY
hukabiliwa na shida au tatizo. Tatizo hilo ni kama lile linaloweza kumkabili
mtu yeyote. Ijapokuwa mhusika huyo hujitahidi kulitatua tatizo hilo, hali ya
ulimwenguni na tabia ya kibinadamu humfanya asiweze kufaulu, na mwishowe
hushindwa. Kwa hiyo, mwisho wa tamthiliya hizi ni masikitiko, maanguko na
hasara kwa mhusika mkuu au jamii. Mfano wa tanzia ni tamthiliya ya Kinjeketile
(Hussein, 1969) na Kifo Kisimani (wa Mberia, 2001).
(b) Ramsa
Ramsa, ambayo hujulikana pia kama komedia au futuhi, hukusudia kufurahisha
au kuchekesha, na huwa na mwisho mwema. Sifa ya kufurahisha na kuchekesha
haimaanishi kwamba tamthiliya za aina hii hazina maudhui mazito. Tamthiliya
hizi hushughulikia masuala mbalimbali ya msingi kama vile uzembe, uzalishaji
mali, siasa, mapenzi na ndoa. Utani, mzaha na kejeli hutumika katika kuchekesha.
Kupitia uchekeshaji huo, jamii, watawala na watu binafsi hukosolewa. Mhusika
mkuu wa ramsa si lazima awe mtu maarufu. Anaweza kuwa mtu wa kawaida
au anaweza kuwa mtu wa nasaba duni, lakini hubeba matendo ya ucheshi
yanayobeba maana nzito. Mhusika huyu akifanikiwa, wasomaji au watazamaji
hufurahi. Mfano mzuri wa ramsa ni tamthiliya ya Mfalme Juha (Topan, 1971) na
Aliyeonja Pepo (Topan, 1973).
(c) Tanzia ramsa
Hii ni tamthiliya yenye mseto wa maudhui ya kuhuzunisha na kufurahisha. Mifano
ya tamthiliya hizi ni Kaptula la Marx (Kezilahabi, 1999), Pambo (Muhando,
1975), Masaibu ya Ndugu Jero (Soyinka, [mf.] Yahaya, 1974), Mabepari wa
Venisi (Shakespeare [mf.] Nyerere, 1969), Wakati Ukuta (Hussein, 1967) na
Amezidi (Mohamed, 1995).
(d) Melodrama
Melodrama ni tamthiliya yenye matumizi mengi ya muziki na uimbaji wa nyimbo.
Inafanana sana na tanzia ingawa, mara nyingi, nguli wa melodrama huibuka na
ushindi. Dhamira za melodrama huzungumzia mvutano kati ya wema na uovu
au ubaya. Matukio yake husisimua sana na mwendo wa msuko wake huwa wa
harakaharaka. Wahusika wake huvutia lakini hawana sifa za kishujaa. Aghalabu,
mwishoni, mhusika mwema huweza kupata ushindi.
42 Kitabu cha Mwanafunzi
Kidato cha Tano
23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 42 23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 42