Page 58 - Fasihi_Kisw_F5
P. 58
Fasihi ya Kiswahili kwa Shule za Sekondari
kazi zilizosawiri maisha yaliyopita. Mfano wa riwaya za kundi hili ni Mtu ni Utu
(Mhina, 1971) na Njozi za Usiku (Seme, 1976). Kundi la pili ni lile lililouona
ujamaa kwa jicho la matarajio kwamba kuna ujenzi wa jamii mpya itakayoishi
vizuri kuliko jamii iliyokuwapo. Kwa hiyo, kundi hili liliandika kazi kwa shauku
FOR ONLINE READING ONLY
ya kueleza mabadiliko yatakayoletwa na vijiji vya ujamaa. Mfano wa riwaya
hizo ni Shida (Balisidya, 1975) na Ndoto ya Ndaria (Ngomoi, 1976). Riwaya
hizi zililenga kuonesha ubora wa maisha ya vijijini. Muundo wa riwaya hizi ni
wa moja kwa moja, lugha nyepesi na wahusika wasio na utata.
Pia, katika kipindi hiki, walijitokeza waandishi walioandika riwaya kwa jicho
la kiyakinifu. Riwaya za namna hii ziliyasawiri masuala ya kijamii kipembuzi.
Mifano ya riwaya hizo ni Kasri ya Mwinyi Fuad (Shafi, 1978), Kuli (Shafi, 1979)
na Dunia Mti Mkavu (Mohamed, 1979). Waandishi wa riwaya hizi wanaeleza
mapambano dhidi ya umwinyi na ubepari. Katika riwaya ya Kasri ya Mwinyi
Fuad, kwa mfano, kuna mvutano baina ya mamwinyi, watwana na watumwa.
Pande hizi mbili zinakinzana na hatimaye, mikinzano inazaa mapinduzi. Kwa
kiasi, waandishi hawa waliathiriwa na fikra za Ki-Marx (Senkoro, 1984).
Katika miaka ya 1980, liliibuka wimbi la uandishi wa riwaya pendwa. Riwaya
hizi zilizuka kutokana na sababu za kiuchumi, ambapo uchumi wa Tanzania
uliyumba kutokana na Vita vya Kagera, majanga kama ukame, pamoja na
masharti magumu ya Shirika la Fedha la Kimataifa na Benki ya Dunia. Waandishi
wengi walianza kuandika riwaya pendwa kwa lengo la kujipatia fedha za haraka.
Pia, zilizuka kampuni nyingi za uchapishaji nchini. Kampuni hizo zilirahisisha
uchapishaji wa riwaya pendwa kwa haraka na kwa gharama nafuu. Soko la
riwaya pendwa lilikuwa kubwa kutokana na maudhui yake kupendwa na watu
wa rika zote. Aidha, waandishi ndio walikuwa wachapishaji na wauzaji wakuu
wa riwaya hizo. Miongoni mwa riwaya hizo ni Tutarudi na Roho Zetu (Mtobwa
1987), Roho Mkononi (Rajab,1984), Dimbwi la Damu (Mtobwa, 1984), Kikomo
(Musiba, 1980) na Njama (Musiba, 1981). Nyingine ni Kijasho Chembamba
(Ganzel, 1980), Ufunguo wa Bandia (Rajab, 1974), Jeraha la Moyo (Kiango,
1974) na Kwa Sababu ya Fedha (Simbamwene, 1972).
Pia, katika kipindi hiki waandishi wengi waliandika riwaya zilizohakiki
jamii. Riwaya hizi zilitokana na Azimio la Arusha kutokukidhi matarajio ya
Watanzania. Wasanii waliandika riwaya kueleza maoni yao kuhusu viongozi
walioaminika kuwaongoza wananchi kuyafikia malengo ya vijiji vya ujamaa.
Viongozi waligeuka wasaliti, waroho, na wazembe huku wakiendekeza rushwa,
uvivu, ulevi na ubadhirifu wa mali ya umma. Mfano wa riwaya za kipindi hicho
Kitabu cha Mwanafunzi 47
Kidato cha Tano
23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 47 23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 47