Page 62 - Fasihi_Kisw_F5
P. 62
Fasihi ya Kiswahili kwa Shule za Sekondari
(k) Riwaya za kimaadili
Hizi ni riwaya zenye nia ya kufundisha maadili fulani yahusuyo mwenendo
mwema katika maisha. Ni riwaya zinazowapa watu maadili, na mara nyingi,
maadili hayo huwa ya kidini. Wahusika wakuu huwa na sifa na tabia nzuri bila
FOR ONLINE READING ONLY
udhaifu. Sifa hizo ni za kudumu; kama ni mwenendo mwema huwa mwema tangu
mwanzo hadi mwisho wa hadithi. Mabadiliko yakitokea, huwa ya kimaadili na
hutokea ghafla. Mifano ya riwaya za aina hii ni Adili na Nduguze (Robert, 1952)
Kisa cha Mrina Asali na Wenzake Wawili (Mnyampala, 1961) na Mtu ni Utu
(Mhina, 1971).
(l) Riwaya za kimapinduzi
Hizi ni riwaya zinazojadili matatizo yanayosababisha migogoro fulani katika
jamii kwa lengo la kuleta mabadiliko. Mabadiliko hayo huweza kuwa ya kisiasa,
kiutamaduni au kiuchumi. Aghalabu, lengo la riwaya hizi ni kuuwezesha umma
kushika hatamu kwa njia ya mapambano. Mifano ya aina hii ya riwaya ni Ubeberu
Utashindwa (Kiimbila, 1971), Kasri ya Mwinyi Fuadi (Shafi, 1974), Kabwela
(Saffari, 1976), Dunia Mti Mkavu (Mohamed, 1979) na Kuli (Shafi, 1979).
(m) Riwaya za kifalsafa
Riwaya za kifalsafa ni zile zinazojadili masuala anuai kuhusu maisha. Aghalabu,
masuala hayo ni yale yanayohitaji tafakuri ya kina. Hii inamaanisha kuwa riwaya
hizi zinajadili kwa kina na kwa kufanya tafakuri makini kuhusu mambo ambayo
hayaonekani kwa urahisi. Muundo wa riwaya hizi ni changamani. Riwaya hizi
hujadili maswali kuhusu maana ya ukweli, maisha au kifo kama vile ukweli ni
nini? Maisha ni nini? Kifo ni nini? Kuwapo na kutokuwapo ni nini? Mifano
ya riwaya za kifalsafa ni Mzingile, Kichwamaji (Kezilahabi, 1974), Dunia
Uwanja wa Fujo (Kezilahabi, 1978), Mafuta (Mkangi, 1984), Kiza katika Nuru
(Mohamed, 1988), Nagona (Kezilahabi, 1989), Ziraili na Zirani (Mkufya, 1999),
na Babu Alipofufuka (Mohammed, 2001).
(n) Riwaya za vitisho
Hii ni riwaya yenye visa vya kutisha na kusisimua. Mara nyingi, visa hivyo
huambatana na mambo ya ajabu au miujiza. Mambo hayo ni kama vile mauaji
ya kishirikina, uchawi, uganga na vita. Mifano ya riwaya hii ni Mbojo Simba
Mtu (Kuboja, 1971), Mirathi ya Hatari (Mung’ong’o, 1977) na Janga Sugu
la Wazawa (Ruhumbika, 2002). Kwa mfano riwaya ya Mirathi ya Hatari,
imeeleza visa na mikasa ya kisihiri katika jamii za Njombe. Msanii amemtumia
Gusto ambaye anarithishwa mirathi ya hatari (uchawi) kutoka kwa baba yake,
Kazembe. Mirathi hiyo inasababisha vifo visivyokuwa vya kawaida. Miongoni
Kitabu cha Mwanafunzi 51
Kidato cha Tano
23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 51 23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 51