Page 63 - Fasihi_Kisw_F5
P. 63
Fasihi ya Kiswahili kwa Shule za Sekondari
mwa vifo hivyo ni kile cha mama yake Gusto, dada yake (Nandi) na mjomba
wake Gusto (Kapedzile). Kuwapo kwa matukio mengi ya kichawi kunaleta hofu
kwa wasomaji wa riwaya hii. Zaidi, matendo yanayotendeka wakati Gusto akila
kiapo cha uchawi yanatisha mno.
FOR ONLINE READING ONLY
(o) Riwaya za watoto na vijalunga
Riwaya za watoto na vijalunga hutofautiana na riwaya za watu wazima kwa
sifa kadhaa, zikiwamo za aina za wahusika, muundo, msuko, uchache wa visa,
michoro na picha, matumizi ya fantasia na fonti zinazotumika. Vilevile, riwaya za
watoto huepuka kusawiri matukio hasi kama vile ya mauaji, masuala ya ngono,
na mahusiano ya jinsia moja. Mifano ya riwaya hizo ni Safari ya Prospa (Lema,
1995), Kimbia Helena Kimbia (Mnyaka, 1995), Moto wa Mianzi (Mulokozi,
1996) na Marimba ya Majaliwa (Semzaba, 2008).
2. Riwaya pendwa
Riwaya pendwa ni zile ambazo hutumia fani inayojichomoza na kusisimua zaidi
kiasi cha kuweza kufunika maudhui. Hali hii huifanya riwaya hizi zionekane kuwa
na lengo la kustarehesha au kuburudisha wasomaji tu. Mambo yanayosawiriwa
sana na waandishi wa riwaya za kundi hili ni mapenzi, upelelezi, ujasusi, ugaidi,
ujambazi na mauaji. Waandishi wa riwaya pendwa huyasawiri mambo hayo kwa
ufundi mkubwa; na hupangilia visa na vituko kwa namna inayosisimua. Nchini
Tanzania, aina hii ya riwaya iliandikwa kwa mara ya kwanza na Muhamed Said
Abdulla (MSA) alipoandika riwaya ya Mzimu wa Watu wa Kale (1957). Mifano
mingine ya riwaya hizi ni Simu ya Kifo (Katalambula, 1965), Kisima cha Giningi
(Abdulla, 1968) na Njama (Musiba, 1981). Uandishi wa riwaya za aina hii
uliongezeka maradufu katika miaka ya 1980, kutokana na matatizo ya kiuchumi.
Sifa za riwaya pendwa
Riwaya pendwa zina sifa zifuatazo:
(i) Hutumia taharuki kwa kiasi kikubwa
Taharuki ni hamu kubwa anayokuwa nayo msomaji kutaka kujua mambo
yatakayotokea na yatakavyotokea katika hadithi. Taharuki hutumiwa kwa kiasi
kikubwa katika riwaya pendwa kupitia matukio ya kusisimua yanayojibainisha
kupitia migogoro iliyosukwa kwa ufundi. Taharuki inafikia kilele wakati fumbo
linapofumbuliwa kwa kujibiwa maswali kadhaa yaliyojitokeza akilini mwa
msomaji. Kwa mfano, katika riwaya ya Mzimu wa Watu wa Kale (Abdulla, 1957)
swali linalojitokeza ni: nani amemuua Bwana Ali Bomani? Mbinu za awali za
52 Kitabu cha Mwanafunzi
Kidato cha Tano
23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 52 23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 52