Page 60 - Fasihi_Kisw_F5
P. 60
Fasihi ya Kiswahili kwa Shule za Sekondari
(a) Riwaya za kijamii
Hizi ni riwaya zinazosawiri maisha na matatizo ya kawaida ya kijamii. Matatizo
hayo huweza kuwa ya kifamilia, kimahusiano, kitabaka, kisiasa na kiutamaduni.
Maudhui mengine ni mgongano kati ya ukale na usasa, kati ya maisha ya mjini na
FOR ONLINE READING ONLY
ya vijijini na migogoro ya kifamilia. Wahusika wake, aghalabu, huwa halisi ambao
wanapatikana katika jamii. Hivyo, huifanya riwaya iwe inaishi wakati wote,
yaani haichuji. Aina hii ndiyo yenye idadi kubwa ya riwaya. Mifano ya riwaya za
aina hii ni Siku ya Watenzi Wote (Robert, 1968), Rosa Mistika (Kezilahabi, 1971),
Titi la Mkwe (Banzi, 1972) na Nyota ya Rehema (Mohamed, 1978).
(b) Riwaya za kisaikolojia
Hizi ni riwaya zinazosaili nafsi ya mhusika. Hudodosa fikra, hisia, mawazo, imani,
hofu, mashaka, matumaini na matamanio ya mhusika binafsi. Vilevile, hudadisi
athari za mambo hayo kwa mhusika na labda jamii yake. Hueleza mikinzano
ya ndani ya mhusika kinafsi, kiakili na kijinsia. Baadhi ya riwaya za aina hii ni:
Rosa Mistika (Kezilahabi, 1971), Kiu (Mohamed, 1972), Ukiwa (Mkangi, 1973),
Kichwamaji (Kezilahabi, 1974), Tata za Asumini (Mohamed, 1990), na Mhanga
Nafsi Yangu (Mohamed, 2012).
(c) Riwaya za sira
Hizi ni riwaya ambazo husimulia habari za maisha ya mtu. Riwaya za aina hii
zimegawanyika katika makundi mawili: riwaya za kitawasifu na za kiwasifu.
(d) Riwaya za kitawasifu
Riwaya za kitawasifu ni zile zinazotumia nafsi ya kwanza, yaani mwandishi
anaelezea mwenyewe kuhusu maisha yake tangu kuzaliwa kwake hadi muda
wa kuandika riwaya husika; au hueleza kipande cha maisha yake ambacho sio
lazima kiwe hadi anapoandika. Mwandishi hueleza matukio ambayo huona
yanasisimua na huenda hayatokei kwa wengine. Kwa kuyaeleza, anadhani
yanaweza kuwasaidia wasomaji. Riwaya ya aina hii huweka kumbukumbu au
historia ya maisha ya mtu binafsi. Mifano ya riwaya za aina hizi ni Maisha Yangu
na Baada ya Miaka Hamsini (Robert, 1949 na 2003), Mbali na Nyumbani (Shafi,
2013) na Nasikia Sauti ya Mama (Walibora, 2015).
(e) Riwaya za kiwasifu
Riwaya za kiwasifu ni zile zinazotumia nafsi ya tatu, yaani mwandishi husimulia
maisha ya mtu mwingine. Mfano wa riwaya za wasifu ni Wasifu wa Siti Binti
Saad (Robert, 1967).
Kitabu cha Mwanafunzi 49
Kidato cha Tano
23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 49 23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 49