Page 69 - Fasihi_Kisw_F5
P. 69
Fasihi ya Kiswahili kwa Shule za Sekondari
Mchango wa fasihi simulizi katika maendeleo ya fasihi andishi
Maendeleo ya fasihi andishi kabla ya uhuru yana uhusiano mkubwa na
wamisionari na watawala wa kigeni. Wageni hawa walipofika pwani ya Afrika
Mashariki, waliwakuta wenyeji wakiwa na fasihi yao. Kwa mfano, baadhi
FOR ONLINE READING ONLY
ya tenzi za zamani kama vile Fumo Liyongo zilikuwa zikisimuliwa kabla ya
maandishi na ziliwekwa katika maandishi baadaye. Pia, tenzi hizi zilitokana na
nyimbo ambazo ndizo fasihi ya awali.
Halikadhalika, kuna athari za mashairi na fani nyinginezo kama tarihi, masimulizi
ya wasafiri, ngano na hekaya mbalimbali. Ngano na hekaya hizi ndizo zilitafsiriwa
na kuwa msingi wa hadithi za awali za Kiswahili. Miongoni mwa hadithi hizo
ni Swahili Tales as Told by the Natives of Zanzibar (1870) zilizotafsiriwa na
Edward Steere. Ngano nyingine zimechapishwa katika Kitabu cha Prosa und
Poesie der Suaheli (1907) kilichohaririwa na Carl Velten, Mazungumzo ya Alfu
Lela Ulela Juzuu (1-4) (1928) kilichotafsiriwa na Edwin Brenn na kuhaririwa na
Frederick Johnson na Hekaya za Abunuwasi (Chiponde, 1928). Kisiwa chenye
Hazina (Johnson, 1929), Safari za Gulliver (Swift, 1932), Mashimo ya Mfalme
Suleimani (Haggard, 1937) na Safari ya Msafiri (Bunyan, 1925).
Kama ulivyojifunza kuhusu tanzu na vipera vya fasihi simulizi, fasihi hii
inajumuisha hadithi, semi, ushairi na sanaa za maonesho na vipera vyake. Baadhi
ya tanzu hizi hujitokeza katika fasihi andishi kwani vipengele mbalimbali vya
tanzu hizo huweza kutumika kama mbinu za kisanaa katika kazi za fasihi andishi.
Mfano wa vipengele hivyo ni wahusika wasio binadamu kama vile wanyama,
mashetani na mazimwi, kama wanavyojitokeza katika riwaya za vitisho na za
kingano. (Senkoro, 2011).
Kuanzia miaka ya 1940 hadi 1960, riwaya nyingi za Kiswahili zilifuata mkondo
wa hekaya na ngano. Kimaudhui, riwaya hizo zilielezea mambo ya mila na
desturi kama njia ya kutunza maadili. Mifano ya riwaya hizo ni Adili na Nduguze
(Robert, 1952), Kusadikika (Robert, 1991) na Kufikirika (Robert, 1968).
Kimsingi, fasihi simulizi imekuwa nguzo ya fasihi andishi katika kueneza
tamaduni mbalimbali za kijamii. Waandishi mbalimbali wamechota fikra kutoka
katika kazi mbalimbali za kifasihi simulizi na kuzitumia katika tungo za fasihi
andishi.
Shughuli ya 2.17
Chunguza vipindi vya fasihi simulizi vinavyorushwa na vituo vya runinga
au sikiliza vipindi kutoka katika vituo viwili vya redio, kisha eleza athari
zinazotokana na vipindi hivyo kurushwa kwa njia hizo.
58 Kitabu cha Mwanafunzi
Kidato cha Tano
23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 58
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 58 23/06/2024 17:54