Page 73 - Fasihi_Kisw_F5
P. 73
Fasihi ya Kiswahili kwa Shule za Sekondari
kwa vijana kusimamia kile wanachokiamini. Mhusika Kalenga alisimama kidete
kufichua uozo uliomo kwenye jamii, na hatimaye alipandishwa cheo kutokana na
kazi nzuri aliyoifanya. Vilevile, kazi nyingine za fasihi kama nyimbo zimekuwa
zikitumika kutia hamasa ya wanawake kufanya kazi ili kujiletea maendeleo bila
kuwa wategemezi katika jamii.
FOR ONLINE READING ONLY
(g) Kukosoa jamii
Fasihi ina mchango katika kukosoa jamii kuhusiana na mambo mbalimbali ya
maisha. Kwa mfano, katika riwaya ya Kufikirika (Robert, 1968), mwandishi
anakosoa tabaka tawala linalotumia rasilimali nyingi kwa manufaa ya watu
wachache ilihali wanajamii wengine wanateseka. Halikadhalika, methali
katika fasihi hutumika kukosoa au kuonya jamii. Methali kama vile “Mkataa
pema, pabaya panamwita” inakosoa mtu anayekataa wosia mzuri kwani kuna
madhara yanaweza kumpata. Aidha, methali kama “Tamaa mbele, mauti nyuma”
imekusudiwa kuwaonya wanajamii kuepuka tamaa kwani mtu mwenye tamaa
anaweza kukabiliwa na madhara.
(h) Kukomboa jamii
Fasihi simulizi na fasihi andishi imechangia sana kupiga vita masuala mbalimbali
yanayokwamisha maendeleo ya jamii kama vile ujinga, maradhi na umaskini.
Tamthiliya ya Hawala ya Fedha (Lihamba, 1985), kwa mfano, inaeleza mambo
yanayosababisha umasikini ambayo ni ujinga na uvivu. Aidha, wakati wa harakati
za ukombozi Kusini mwa Afrika, baadhi ya bendi za muziki wa dansi zilipiga
nyimbo za kuwaunganisha watu kwa ajili ya ukombozi. Mfano mzuri wa wimbo
wa “Mwenyekiti Mwalimu Nyerere” ulioimbwa na bendi ya Urafiki Jazz miaka
ya 1970 wimbo huo ulikuwa ukimsihi mwenyekiti wa nchi tano zilizo mstari wa
mbele kupigania ukombozi wa Kusini mwa Afrika azidishe mapambano kwani
maadui wa Afrika walilisumbua sana Bara la Afrika.
Shughuli ya 2.19
(a) Kwa kutumia vyanzo mbalimbali, jadili mchango wa fasihi andishi ya
Kiswahili katika jamii.
(b) Jadili uhusiano uliopo baina ya fasihi simulizi na fasihi andishi.
Tamrini
1. Kwa kutumia mifano, eleza namna sayansi na teknolojia zinavyochangia
katika kukuza fasihi simulizi na andishi.
2. Fafanua tofauti kati ya maigizo na tamthiliya andishi ya Kiswahili.
62 Kitabu cha Mwanafunzi
Kidato cha Tano
23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 62
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 62 23/06/2024 17:54