Page 76 - Fasihi_Kisw_F5
P. 76
Fasihi ya Kiswahili kwa Shule za Sekondari
Wataalamu hawa huitazama fani na maudhui kama chungwa na ganda lake au
kikombe na chai.
Zifutazo ni hoja za mtazamo wa kidhanifu:
FOR ONLINE READING ONLY
(a) Fani na maudhui ni kama chungwa na ganda lake: Mtazamo huu
unayaona maudhui kama nyama ya ndani ya chungwa na fani ni ganda
lake la nje ambalo huifunika nyama hiyo. Mtu anapotaka kula chungwa
huliondoa ganda lake na kulitupa, kwani lengo huwa ni kuipata nyama ya
ndani. Kwa mtazamo huu, fani na maudhui huweza kutenganishwa. Hivyo,
mtunzi anapotunga kazi yake huwa hana haja na fani kwani kusudi lake ni
maudhui ambayo hulengwa kwa hadhira husika. Maudhui lengwa huweza
kuifikia jamii hata kama hayajafumbatwa na fani. Hadhira inaposoma kazi
hiyo hutafuta maudhui na si fani iliyoifunika kazi hiyo.
(b) Fani na maudhui kama kikombe na chai: Mtazamo huu umejitokeza
katika kazi za baadhi ya watalaamu wa fasihi. Miongoni mwao ni
Nkwera (1978) ambaye anashadidia kuwa fani na maudhui vinaweza
kutenganishwa na kwamba kila kimoja kinajitegemea kama ilivyo kikombe
na chai. Kikombe hutumika kubeba chai ili mnywaji aweze kuinywa. Chai
ikinyweka kikombe huwa hakina kazi tena. Hapa kikombe kinawakilisha
fani na chai ni maudhui katika kazi za fasihi. Hii ina maana kuwa mtunzi
wa kazi ya fasihi hulenga kufikisha maudhui kwa jamii na fani huwa ni
kibebeo chake tu. Mtazamo huu unaona kuwa mtunzi anaweza kufikisha
maudhui kwa hadhira yake bila kutumia fani.
Mtazamo wa kiyakinifu
Mtazamo wa kiyakinifu huitazama fani na maudhui kama vipengele
vinavyotegemeana na ambavyo haviwezi kutenganishwa. Hii ni kwa sababu fani
na maudhui hutegemeana, huathiriana na kujengana. Mtazamo huu hulinganisha
fani na maudhui kama pande mbili za sarafu. Ifuatayo ni hoja kuu ya mtazamo
wa kiyakinifu:
Fani na maudhui kama pande mbili za sarafu moja: Mtazamo huu unaungwa
mkono na Senkoro (1982 na 2011) unafananisha fani na upande wa kwanza wa
sarafu, ilhali maudhui ni upande wa pili. Hii ina maana kwamba pande mbili
za sarafu ndizo huikamilisha sarafu hiyo; hivyo, haziwezi kutenganishwa.
Kitabu cha Mwanafunzi 65
Kidato cha Tano
23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 65 23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 65