Page 71 - Fasihi_Kisw_F5
P. 71
Fasihi ya Kiswahili kwa Shule za Sekondari
Matumizi ya simu nayo yana mchango mkubwa katika jamii. Watu wengi hutumia
simu kwa mawasiliano ya mazungumzo. Kuwapo kwa mawasiliano ya mitandao
ya kijamii kwa kutumia simu kumewezesha uwasilishaji na uenezaji wa fasihi
simulizi. Baadhi ya simu zina uwezo wa kurekodi na kutuma nyimbo, masimulizi
na picha. Pia, zina uwezo wa kunasa vituo mbalimbali vya redio na runinga na,
FOR ONLINE READING ONLY
hivyo, kuwawezesha watumiaji wake kusikiliza kazi za kifasihi. Vilevile, vifaa
kama vile vishikwambi, na kompyuta vimerahisisha uhifadhi, ubebaji, na usomaji
wa kazi za fasihi andishi. Zaidi, teknolojia imesaidia kupatikana kwa majukwaa ya
kidijiti kama vile mitandao ya kijamii ambayo watunzi wa kazi za fasihi simulizi
na andishi huitumia kuwasilishia au kuuzia kazi zao.
Kadhalika, kutokana na maendeleo ya kiteknolojia, fasihi simulizi pia imekuwa
ikiwasilishwa kwa njia ya maandishi. Hii inatokana na kuongezeka kwa viwanda
vya uchapaji ambavyo vimerahisisha mchakato wa uzalishaji wa machapisho ya
kazi mbalimbali za fasihi, zikiwamo zinazotokana na fasihi simulizi.
Shughuli ya 2.18
(a) Kusanya semi kumi (10) za Kiswahili kulingana na makundi yafuatayo:
(i) Methali tano (5) zinazoonya kuhusu utovu wa nidhamu.
(ii) Misemo mitano (5) inayohamasisha umoja na ushirikiano katika jamii.
(b) Jadili mchango wa semi ulizozikusanya na umuhimu wake kwa maendeleo
ya jamii.
Mchango wa fasihi simulizi na fasihi andishi katika maendeleo ya jamii
Fasihi simulizi na andishi zimekuwa na mchango mkubwa kwa jamii ambao
umesaidia katika kuigeuza na kuibadilisha jamii. Mchango huo umeweza
kujidhihirisha kama ifuatavyo:
(a) Kuelimisha jamii
Mchango mkubwa wa fasihi simulizi na andishi ni kuelimisha jamii. Fasihi
huufumbua macho umma na kupiga vita matatizo ya njaa, maradhi, umaskini na
mengineyo. Aidha, fasihi huipa jamii maarifa na stadi za kukabiliana na mazingira
ambamo jamii inaishi. Kwa mfano, kuna nyimbo mbalimbali zinazotoa elimu juu
ya utunzaji wa mazingira. Kutokana na nyimbo hizo jamii imeweza kuelimika na
kupata maarifa ya namna ya kutunza mazingira pamoja na kuendeleza shughuli za
maendeleo binafsi na ya kitaifa. Jamii inasisitiza kuwa mazingira yasipotunzwa
husababisha mabadiliko hasi ya tabia nchi.
60 Kitabu cha Mwanafunzi
Kidato cha Tano
23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 60
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 60 23/06/2024 17:54