Page 70 - Fasihi_Kisw_F5
P. 70
Fasihi ya Kiswahili kwa Shule za Sekondari
Athari za sayansi na teknolojia katika maendeleo ya fasihi simulizi na
fasihi andishi
Maendeleo ya sayansi na teknolojia yamesaidia sana katika uwasilishaji na
uenezaji wa fasihi simulizi. Maendeleo haya yamewezesha kuwapo kwa vyombo
mbalimbali vya uwasilishaji kama redio, runinga na simu. Redio na runinga
FOR ONLINE READING ONLY
zimekuwa na mchango mkubwa katika uwasilishaji na uenezaji wa kazi za fasihi
simulizi. Kwa mfano, Redio Tanzania (kwa sasa TBC Taifa) imekuwa na vipindi
ambavyo vimesaidia sana fasihi simulizi kuwafikia watu wengi. Kipindi kama
vile Mama na Mwana kilipendwa na watu wengi, hasa watoto, kwa sababu
ya masimulizi ya hadithi mbalimbali. Kipindi kingine ni Cheichei Shangazi
ambacho kimekuwa na masimulizi ya hadithi, vitendawili na nyimbo. Baadaye,
vilianzishwa vituo vingine vya redio na kuongeza mawanda ya uwasilishaji
na uenezaji wa kazi za fasihi simulizi. Kwa mfano, Redio One Stereo hurusha
kipindi cha Watoto Wetu ambacho hupambwa na wimbo maarufu wa “Watoto
Wasafi Moyoni”. Kipindi hiki hurushwa kila Jumamosi, ambapo watoto walioko
studio na nyumbani huweza kushiriki katika uwasilishaji wa hadithi, methali,
vitendawili, mafumbo na nyimbo.
Pamoja na watoto kutoonana ana kwa ana, wanaweza kushiriki kwa njia ya
kusikiliza. Hivyo, hadithi ambazo awali zilisimuliwa kwa watu wachache,
zinaweza kujulikana kwa wote wanaosikiliza. Mbali na vipindi vya watoto, redio
zimekuwa zikirusha vipindi vingine vya fasihi simulizi. Baadhi ya vipindi hivyo
ni Mkoa kwa Mkoa, Malenga Wetu, Ngoma Zetu, Zilipendwa, (TBC Taifa), Hizi
Nazo (Redio One Stereo), Kwa Raha Zetu (Redio Clouds FM) na Mitikisiko ya
Pwani (Times FM).
Kwa upande wa runinga, uwasilishaji umekuwa tofauti kidogo. Katika runinga
washiriki wana fursa ya kuona matendo yanayotendwa. Kuna vipindi vya watoto
ambavyo huwasilisha kazi za fasihi simulizi. Mfano wa vipindi hivyo ni kipindi
cha Watoto kilichoandaliwa na TET ambacho hurushwa na TBC1 na TBC2. Kipindi
hiki kinachorushwa siku za Jumamosi na Jumapili, husimulia hadithi na michezo
ya watoto. Pia, kuna kipindi cha Ubongo Kids (TBC1) ambacho kinahusu somo
la hisabati na kusoma. Kipindi hiki huwa na matumizi ya nyimbo, usimulizi wa
hadithi, na maigizo mbalimbali. Aidha, kituo cha ITV hurusha kipindi cha Watoto
Show ambacho hujumuisha nyimbo, ngoma, methali, vitendawili na hadithi.
Halikadhalika, runinga zimekuwa zikirusha vipindi kama vile, Mizengwe, Sanaa
na Msanii, Mashamushamu ya Pwani na Hawavumi lakini Wamo (ITV). Vipindi
vingine ni Futuhi, Bongo Beats na Msanii Wetu (Star TV). Aidha, kuna Fataki,
Ngoma Zetu, Mchikicho wa Pwani Club Raha Leo Show (TBC1), na Mirindimo
ya Pwani (Channel Ten). Vipindi vyote hivyo vimekuwa vikisaidia uwasilishaji
na uenezaji wa fasihi simulizi.
Kitabu cha Mwanafunzi 59
Kidato cha Tano
23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 59 23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 59