Page 85 - Fasihi_Kisw_F5
P. 85
Fasihi ya Kiswahili kwa Shule za Sekondari
Shughuli ya 3.10
Kwa kutumia vyanzo vya mtandaoni na maktabani, fafanua maana na misingi ya
nadharia ya mwitiko wa msomaji katika kuhakiki kazi za fasihi.
FOR ONLINE READING ONLY
Nadharia ya mwitiko wa msomaji
Nadharia ya mwitiko wa msomaji huhusu namna msomaji anavyoikabili,
anavyoifasili na kuipa kazi ya fasihi maana kutokana na tajriba yake.
Mmoja wa waasisi wa nadharia hii ni Wolfgang Iser (1926 - 2007) ambaye
anajulikana kama baba wa nadharia hii.
Kwa kawaida, mwandishi anapoandika kazi yake hutawaliwa na mambo kama
vile mazingira, historia au muktadha wa jamii yake. Kwa upande mwingine,
msomaji wa matini naye huathiriwa na mambo kama vile uelewa binafsi, aina
ya matini anayosoma, utamaduni, mtindo wa usomaji, uzoefu wake juu ya
jambo analolisoma, mazingira, historia, na matarajio yake. Mambo haya ndiyo
husababisha tofauti ya uelewekaji wa matini baina ya msomaji mmoja na
mwingine. Kwa hiyo basi, nadharia hii huhusisha mambo matatu: mtunzi wa
kazi ya fasihi, kazi husika ya fasihi, na hadhira. Pia, husisitiza kuwa hadhira
hukamilisha maana kwa sababu msomaji ndiye anayelengwa na mwandishi; pia
maana ya matini inategemea namna msomaji atakavyoelewa.
Misingi ya nadharia ya mwitiko wa msomaji
Ifuatayo ni misingi ya nadharia ya mwitiko wa msomaji:
(i) kazi ya fasihi haina maana moja;
(ii) maana ya kazi ya fasihi hukamilishwa na miktadha mbalimbali inayotokana
na tajriba ya msomaji;
(iii) mchakato wa usomaji na uelewaji wa kazi ya fasihi huhusisha matarajio ya
msomaji; na
(iv) tofauti za kitamaduni, kielimu, kisiasa, na kiuchumi husababisha tofauti za
maana ya kazi ya fasihi kati ya msomaji mmoja na mwingine.
Unapohakiki kazi ya fasihi kwa kutumia nadharia ya mwitiko wa msomaji
unatakiwa kuzingatia misingi iliyobainishwa.
74 Kitabu cha Mwanafunzi
Kidato cha Tano
23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 74 23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 74