Page 87 - Fasihi_Kisw_F5
P. 87
Fasihi ya Kiswahili kwa Shule za Sekondari
Mpaka hapa umejifunza baadhi ya nadharia muhimu zinazotumika katika uhakiki
wa kazi za fasihi. Nadharia hizi zitakupa mwongozo katika kuchambua kazi
mbalimbali za kifasihi.
Shughuli ya 3.12
FOR ONLINE READING ONLY
Kwa kutumia vyanzo vya mtandaoni na maktabani, eleza sifa na dhima za
mhakiki wa kazi za kifasihi.
Kuhakiki kazi za fasihi kwa kutumia nadharia za kifasihi
Taaluma ya uhakiki ilianza zamani, tangu enzi za mwanafalsafa wa zamani wa
Kiyunani, Plato, (takribani miaka ya 428 - 348 K.K). Nchini Tanzania, taaluma
hii ilianza kutumika zaidi miaka ya 1970 baada ya baadhi ya Watanzania kusoma
taaluma ya fasihi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Miongoni mwao
walikuwa John Ramadhani, May Balisidya, Saifu Kiango, Euphrase Kezilahabi,
na Mbunda Msokile. Wengine ni pamoja na Farouk Topan, Tigiti Sengo, Fikeni
Senkoro na Mugyabuso Mulokozi.
Unapohakiki kazi ya fasihi unachambua na kutathmini mawazo au masuala
mbalimbali yaliyomo katika kazi hiyo. Mbali na kuwa na maarifa ya nadharia
zinazoongoza katika kuchambua kazi za fasihi, unapaswa kufahamu historia
na siasa ya jamii inayohusika ili uweze kuelewa masuala muhimu katika jamii
husika. Halikadhalika, inakulazimu kusoma kazi nyingine za fasihi tofauti
na ile unayoihakiki ili uwe na ujuzi zaidi katika uwanja wa uhakiki. Vilevile,
unapohakiki kazi za fasihi ni muhimu kujua historia na mazingira yaliyomkuza
mwandishi au msanii; na mwisho kueleza bayana ubora na upungufu wa kazi
husika.
Ukiwa na ufahamu wa kutosha kuhusu nadharia, itakuwia rahisi kuamua ni
nadharia gani uitumie katika kuhakiki kazi fulani ya fasihi. Uteuzi wa nadharia
ya kutumika hutegemea mwelekeo wa jumla wa kazi inayohakikiwa pamoja na
kipengele au vipengele mahususi unavyotaka kuvifanyia uhakiki.
Kumekuwa na mjadala kuhusu nafasi ya mhakiki wa kazi za fasihi. Mjadala huu
umetokana na kuwapo kwa mitazamo miwili inayopingana kuhusu nafasi ya
mhakiki huyo. Mtazamo wa kwanza unaona kwamba msanii na mhakiki ni watu
ambao wanahitajiana kwa sababu mhakiki ndiye anayeieleza na kuitambulisha
kazi ya msanii kwa hadhira. Vilevile, mhakiki ndiye anayemtahadharisha
mwandishi kuhusu makosa aliyoyafanya ndani ya kazi yake na kumfanya awe
makini zaidi katika kushughulikia kazi nyingine. Aidha, mhakiki ni kiungo
muhimu kati ya jamii na msanii kwa sababu hutumia ujuzi wake wa kuchambua
76 Kitabu cha Mwanafunzi
Kidato cha Tano
23/06/2024 17:54
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 76
FASIHI YA KISWAHILI KITABU CHA MWANAFUNZI KIDATO CHA TANO.indd 76 23/06/2024 17:54