Page 17 - Historia_Maadili
P. 17
Mfanyabiashara maarufu wa Kiarabu katika njia hii ya kati alikuwa Hemed bin
Muhammad bin Juma bin Rajab el Murjebi, maarufu kama “Tippu Tip”. Njia kuu ya
tatu ilikuwa ya Kusini. Njia hii ilianzia Kilwa Kivinje kuelekea Ziwa Nyasa, kaskazini
mwa Msumbiji, Malawi na mashariki mwa Zambia. Njia hii ilitawaliwa na Wayao.
Njia hizi zilitumika kupitisha bidhaa mbalimbali pamoja na misafara ya watumwa.
FOR ONLINE READING ONLY
Ukuaji wa kilimo cha mazao ya biashara kama karafuu katika visiwa vya Pemba
na Unguja na kilimo cha miwa huko Komoro, Ngazija, Mauritius na Reunion,
ulisababisha ongezeko kubwa la mahitaji ya watumwa kutoka maeneo mbalimbali,
hasa Tanganyika. Hii ilichangia kukua kwa biashara ya utumwa katika maeneo mengi
ya eneo hili.
Kwa ujumla, katika kipindi cha utawala wa Waarabu, uchumi ulikuwa wa kinyonyaji,
kwani Waarabu walikuwa wanufaika wakuu wa mapato, huku Waafrika wengi
wakinyonywa kwa kufanya kazi kwa ujira mdogo na wengine wakigeuzwa kuwa
watumwa. Watumwa hawa waliuzwa na wengine kutumikishwa katika mashamba
makubwa ya mikarafuu na minazi ya Waarabu huko visiwani Unguja na Pemba.
Zoezi la 1.2
1. Fafanua namna ambavyo kushamiri kwa biashara kulivyoifanya Zanzibar
kuwa dola kubwa na kitovu cha biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki.
2. Eleza mabadiliko ya kiuchumi yaliyoletwa na Waarabu katika jamii za pwani
ya Tanganyika na Zanzibar.
3. Linganisha thamani ya bidhaa zilizobadilishwa kati ya wafanyabiashara wa
Kiarabu na jamii za pwani ya Tanganyika na Zanzibar.
Mabadiliko ya kijamii wakati wa utawala wa Waarabu
Kabla ya kuwasili kwa Waarabu, jamii za pwani ya Tanganyika na Zanzibar zilijengwa
juu ya maadili yaliyotokana na dini zao za jadi, ambapo baadhi yao waliabudu Mungu
kupitia miti mikubwa, majabali na mapango makubwa, mito, maziwa na bahari na
walitoa kafara kwa malengo mbalimbali kulingana na imani zao. Aidha, jamii hizi
zilijikita katika kutoa elimu ya jadi ambayo ililenga kumpatia kijana maarifa na
ujuzi wa kukabiliana na mazingira yake. Hii ilimwezesha kuishi vyema kwa kufuata
maadili na mila za jamii yake. Kuja kwa Waarabu kulileta mabadiliko makubwa
katika masuala ya elimu, maadili na utamaduni katika jamii hizi.
Jamii za pwani ya Tanganyika na Zanzibar zilijifunza lugha ya Kiarabu ili kuimudu dini
ya Kiislamu na kuendana na matakwa na tamaduni za Waarabu. Hali hii ilisababisha
watu wengi kujiunga na madrasa kwa ajili ya kujifunza dini ya Kiislamu na lugha
9
03/10/2024 18:15:07
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 9
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 9 03/10/2024 18:15:07

