Page 19 - Historia_Maadili
P. 19
Ujerumani ilichukua rasmi mamlaka ya kutawala Afrika Mashariki ya Kijerumani.
Wajerumani walikusudia kuimarisha utawala wao katika koloni hili kwa kuzitumia
mbinu mbalimbali. Mbinu hizo zilijumuisha matumizi ya vyombo vya kiitikadi kama
vile elimu na dini. Mbinu nyingine ilikuwa ni kuunda vyombo vya dola kama jeshi,
magereza na mahakama za kikoloni ili kuhakikisha wananchi hawaupingi utawala
wa kikoloni na wanazitii sheria zilizowekwa. Aidha, walitumia mbinu ya kuwapeleka
FOR ONLINE READING ONLY
watawala wazungu katika ngazi za uongozi na kuondoa tawala za jadi. Kwa ujumla,
ujio wa Wajerumani ulileta mabadiliko makubwa ya kiuchumi, kisiasa na kijamii
katika jamii za Kitanzania.
Mabadiliko ya kiuchumi wakati wa utawala wa Wajerumani
Kama ilivyosemwa awali, lengo kuu la Wajerumani kuja katika Afrika Mashariki ya
Kijerumani lilikuwa kutafuta suluhisho la changamoto za kiuchumi zilizotokana na
mapinduzi ya viwanda, kama vile upungufu wa masoko na malighafi, kwa viwanda
vyao barani Ulaya. Kwa hivyo, kupitia ukoloni, wakoloni waliweza kuzipunguza
changamoto hizo kwa kuanzisha uchumi wa kikoloni ambao ulileta mabadiliko
makubwa kwenye jamii za Kitanzania. Shughuli za uzalishaji mali zilitegemea sana
uzalishaji wa mazao ya biashara kama vile kahawa, chai, mkonge, pamba, tumbaku
na mpira. Mazao haya yalilimwa katika maeneo mbalimbali ya Afrika Mashariki ya
Kijerumani. Kwa mfano, kahawa ililimwa Bukoba, Kilimanjaro, Arusha na Tukuyu;
pamba ilianza kulimwa katika maeneo ya Mwanza, Shinyanga, Morogoro, Bagamoyo,
Rufiji na Lindi; katani ililimwa huko Tanga, Morogoro, Lushoto, Lindi, Dar es Salaam
na Pwani; mpira ulilimwa maeneo ya pwani hasa katika bonde la mto Pangani huko
Tanga na bonde la mto Rufiji hasa maeneo ya Mohoro. Walowezi wa Kijerumani
walianzisha mashamba ya katani yenye ukubwa wa ekari zaidi ya 100,000 (hekta
40,000). Walowezi wengine walipanda zaidi ya miche milioni mbili ya kahawa,
ekari 200,000 (hekta 81,000) za miti ya mipira na mashamba ya pamba. Maeneo ya
Rukwa, Kigoma, Mtwara, Dodoma na Singida hayakuruhusiwa kuanzisha kilimo cha
mashamba makubwa kwa sababu yalitengwa maalumu kwa ajili ya kutoa wafanyakazi
na vibarua (manamba) watakaofanya kazi katika mashamba makubwa ya walowezi
na migodi ya madini hasa dhahabu huko Chunya, Sekenke na Mwanza.
Kwa upande wa viwanda, Wajerumani hawakuanzisha viwanda vikubwa bali
walijenga viwanda vidogo, hasa vya kuchakata malighafi ili kupunguza uzito wake
kabla ya kusafirishwa kwenda Ujerumani. Kwa mfano, walijenga vinu vya kukoboa
kahawa, kuchambua pamba na kusindika mkonge. Wajerumani walijenga viwanda
vidogovidogo vya kuzalisha viatu, viberiti, baruti na risasi. Hivyo, Wajerumani
hawakujenga viwanda vikubwa vya kuzalisha bidhaa mbalimbali za viwandani kama
vile nguo, kamba na mazulia, bali walilenga kurahisisha usafirishaji wa malighafi tu.
Vilevile, Wajerumani waliendesha biashara ya kinyonyaji, kwani koloni hili lilitumika
kama soko la kuuzia bidhaa za viwandani kutoka Ujerumani, kama vile nguo, baiskeli,
11
03/10/2024 18:15:07
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 11 03/10/2024 18:15:07
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 11

