Page 21 - Historia_Maadili
P. 21
Afya
Huduma za afya katika kipindi cha ukoloni zilitolewa kwa ubaguzi wa rangi, ambapo
huduma hizo zilipatikana katika maeneo ambayo wakoloni walianzisha shughuli
kubwa za uzalishaji mali kama vile mashamba na makazi yao. Wazawa walipata
matibabu ya kiwango cha chini ukilinganisha na Wazungu na Waasia. Matibabu haya
yalilenga kuwawezesha Waafrika kuzalisha malighafi bila kusumbuliwa na magonjwa
FOR ONLINE READING ONLY
hasa ya kitropiki au kuumia wakiwa kazini. Aidha, huduma za afya zilitilia mkazo
matibabu badala ya kinga dhidi ya magonjwa. Madhumuni ya kueneza huduma hizi
yalikuwa ni kuhakikisha kwamba wazalishaji mali katika maeneo hayo wanakuwa
na afya njema ili waweze kufanikisha malengo ya kikoloni.
Athari hasi za huduma hizi zilikuwa ni kupotea kwa umaarufu kwa waganga na
matabibu wa jadi, pamoja na dawa zao kushuka thamani. Hii ilisababishwa na
ongezeko la vituo vya matibabu na matumizi ya dawa za kigeni. Hata hivyo, bado
waganga wa jadi waliendelea kutoa matibabu, hasa katika maeneo ya vijijini.
Huduma za maji na umeme
Katika kipindi cha ukoloni, huduma za maji na umeme zilitolewa kwa ubaguzi na
upendeleo, kwani huduma hizi zilielekezwa zaidi katika maeneo yenye umuhimu
wa kiuchumi. Kwa mfano, usambazaji wa huduma hizi ulifanyika katika migodi,
viwandani, maeneo ya mijini, mashamba makubwa ya wakoloni na makazi ya
walowezi wa Kizungu na Kiasia.
Miundombinu ya mawasiliano
Wakoloni walijenga njia za uchukuzi na mawasiliano kama vile barabara, reli na
bandari. Miundombinu hii ilikuwa muhimu kwa usafirishaji wa malighafi, bidhaa
na watu. Reli na barabara zilijengwa kutoka maeneo ya uzalishaji wa malighafi hadi
bandarini. Malighafi kutoka makoloni ilisafirishwa kwenda Ulaya na bidhaa za
viwandani kutoka Ulaya kama vile nguo, vyombo vya nyumbani na zana za chuma
ziliingizwa kupitia bandari hizo na kuletwa Afrika Mashariki ya Kijerumani.
Kazi ya kufanya 1.4
Kwa kusoma matini katika vitabu na mtandaoni, fanya utafiti mdogo kuhusu
tiba za jadi wakati wa ujio wa Wajerumani. Utafiti wako ujikite katika maeneo
yafuatayo:
(a) Namna tiba za jadi zilivyokuwa kabla ya ujio wa Wajerumani;
(b) Magonjwa yaliyotibiwa kwa kutumia tiba za jadi;
(c) Namna Wajerumani walivyoathiri tiba za jadi; na
(d) Toa ushauri kuhusu umuhimu wa tiba za jadi kwa jamii za sasa za
Kitanzania.
13
03/10/2024 18:15:08
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 13 03/10/2024 18:15:08
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 13

