Page 20 - Historia_Maadili
P. 20
mapanga, majembe, viatu na sigara. Bidhaa hizi zote ziliuzwa kwa bei kubwa, wakati
malighafi zilizotumika kuzalisha bidhaa hizo zilinunuliwa kwa bei ndogo sana.
Zoezi la 1.3
FOR ONLINE READING ONLY
1. Fafanua sababu zilizowafanya Wajerumani kuanzisha utawala wa kikoloni
katika jamii za Kitanzania.
2. Kwa nini Wajerumani walijenga viwanda vidogo badala ya viwanda vikubwa
katika Afrika Mashariki ya Kijerumani?
3. Eleza athari ambazo zingetokea iwapo Wajerumani wangejenga viwanda
vikubwa vya kuchakata malighafi katika Afrika Mashariki ya Kijerumani.
Mabadiliko ya kijamii wakati wa utawala wa Wajerumani
Wajerumani walilazimika kujenga na kutoa huduma kadhaa ili kufanikisha malengo
yao katika Afrika Mashariki ya Kijerumani. Huduma hizi zilijumuisha elimu, afya,
maji na umeme, pamoja na miundombinu ya mawasiliano.
Elimu
Elimu iliyotolewa na Wajerumani ililenga kukidhi mahitaji ya shughuli zao za
kikoloni. Mfumo wa elimu uliundwa mahususi ili kuandaa wasaidizi watakaowasaidia
Wajerumani katika shughuli hizo. Elimu hiyo ililenga zaidi wananchi wachache
ambao wangeweza kuzalisha malighafi kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya uchumi wa
kikoloni. Malengo ya elimu hiyo yalikuwa yafuatayo:
(a) Kueneza utamaduni wa Kijerumani;
(b) Kuandaa watumishi wa ngazi za chini;
(c) Kufundisha uadilifu na maadili ya kazi; na
(d) Kuandaa wazalishaji mali kwa ajili ya uchumi wa Kijerumani.
Ili kutimiza malengo hayo, mtaala wa elimu ya Kijerumani ulifundisha stadi kama
vile uashi, useremala, ukarani, upigaji picha, ufundi wa kushona na utengenezaji wa
viatu. Shule mbalimbali zilianzishwa na kugawanywa katika makundi mawili: shule
za Wamisionari na shule za serikali. Hata hivyo, mtaala wa shule za serikali ulipingwa
na Wamisionari ambao walitaka utumike mtaala wa shule zao. Elimu ilitolewa kwa
lugha ya Kiswahili, huku shule za serikali zikihudumia zaidi wavulana na wasichana
wakibaguliwa. Mfumo huu wa elimu ya kikoloni ulikuwa na idadi ndogo ya wanafunzi
wa Kiafrika.
12
03/10/2024 18:15:08
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 12
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 12 03/10/2024 18:15:08

