Page 24 - Historia_Maadili
P. 24
Hata hivyo, wakati Waingereza walipopewa idhini ya kutawala Tanganyika na
Zanzibar, wananchi walikuwa tayari wanajishughulisha na kilimo cha mazao ya
biashara, kama vile buni iliyolimwa Moshi na Bukoba. Pamba nayo ilikuwa ikilimwa
katika maeneo ya Mwanza, Shinyanga, Morogoro na Pwani. Shughuli za biashara
wakati wa utawala wa Waingereza zilifanywa na watu wa jamii ya Kiasia, hasa
Waarabu na Wahindi. Jamii hii ilijihusisha na biashara ya kununua mazao kutoka
FOR ONLINE READING ONLY
kwa wakulima na kuyauza kwa makampuni ya kibepari ya Wazungu. Pia, walifanya
biashara ya kuuza bidhaa mbalimbali zilizoagizwa kutoka Ulaya magharibi na
Marekani. Watanganyika na Wazanzibari hawakuruhusiwa kushiriki katika biashara
wakati wa utawala huo. Waingereza, Wagiriki na Wahindi ndio waliofanya biashara
ya kuagiza na kusafirisha nje ya koloni bidhaa mbalimbali. Waarabu na Wahindi
walifanya biashara ya maduka ya rejareja maeneo ya mijini na vijijini.
Kwa upande wa viwanda, Waingereza hawakuwekeza sana katika viwanda vikubwa
ila walianzisha viwanda vidogo vidogo. Serikali ya Waingereza ilikusanya malighafi
kama vile mazao ya kilimo, madini na mifugo na kuzisafirisha kwenda kwenye
viwanda vyao huko Uingereza. Bidhaa zilizozalishwa huko zililetwa na kuuzwa
kama bidhaa za viwandani hapa nchini. Viwanda vilivyokuwa hapa vilijikita zaidi
katika kuchakata malighafi ili kupunguza uzito kabla ya kusafirishwa. Kwa mfano,
viwanda vya kusindika buni, katani, karanga na pamba, pamoja na viwanda vya
kukaushia tumbaku vilianzishwa. Waingereza pia waliendeleza uchimbaji wa
madini kwa kupanua migodi iliyoachwa na Wajerumani na kuanzisha mingine
mipya, kama migodi ya chumvi huko Uvinza na Ulanga na migodi ya dhahabu
huko Chunya na Geita.
Usafirishaji na uchukuzi ni baadhi ya shughuli za kiuchumi zilizopewa kipaumbele
na serikali ya Waingereza. Juhudi za kufufua miundombinu iliyoharibiwa na vita
zilifanyika, ikiwemo kukamilisha ujenzi wa reli katika baadhi ya maeneo kama vile
reli kutoka Tabora hadi Mwanza na reli kutoka Moshi hadi Arusha. Pia, bandari na
usafiri wa meli katika Ziwa Tanganyika na ziwa Viktoria uliimarishwa. Lengo la
kuimarisha usafirishaji na uchukuzi lilikuwa kurahisisha usafirishaji wa malighafi
kutoka maeneo ya uzalishaji hadi bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara tayari
kwa kusafirishwa Ulaya. Vilevile, njia hizi za usafirishaji ziliwezesha bidhaa za
viwandani kusafirishwa kutoka bandarini kuelekea masoko ya maeneo ya bara.
Kwa upande wa Zanzibar, Waingereza waliwatumia Waarabu na Wahindi kuendeleza
masilahi yao ya kiuchumi. Waarabu walipewa ardhi yenye rutuba kwa ajili ya kilimo
cha mikarafuu na minazi, wakati Wazanzibari wengi walipewa ardhi isiyo na rutuba.
Wahindi walipewa jukumu la kusimamia biashara, hivyo walijenga shule ili kuendeleza
uzoefu wao. Mnamo mwaka 1923, shule kwa ajili ya watoto wa Kihindi zilianzishwa.
16
03/10/2024 18:15:08
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 16 03/10/2024 18:15:08
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 16

