Page 29 - Historia_Maadili
P. 29
kahawa na yale maeneo waliyotokea manamba. Hivyo, miundombinu hiyo wakati
wa utawala wa Waingereza ilisaidia katika kuwasafirisha manamba kwenda kufanya
kazi kwenye mashamba na migodi. Pia, miundombinu ya barabara na reli ilitumika
kusafirisha malighafi kutoka bara hadi bandarini, kusambaza bidhaa za viwandani
kutoka bandarini hadi bara. Vilevile, kusafirisha askari kwenda maeneo yaliyokuwa
na upinzani na hatimaye, kusafirisha watawala kwenda kusimamia shughuli katika
FOR ONLINE READING ONLY
maeneo mbalimbali. Huduma za usafirishaji wakati wa utawala wa Waingereza
hazikulenga moja kwa moja kuwanufaisha Waafrika kama abiria, bali zililenga
kurahisisha mipango na matakwa ya kikoloni ya unyonyaji na ukandamizaji wa
wananchi, pamoja na kusafirisha malighafi kwenda Ulaya kwa ajili ya viwanda vyao.
Huduma za maji na umeme: Serikali ya Uingereza ilijitahidi kuwapa wananchi wa
Tanganyika na Zanzibar huduma za maji na umeme ili kuwawezesha kuwa na afya
bora ili kuendelea kuzalisha malighafi. Baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, serikali
ilipanua huduma hizi, upanuzi ambao ulifanyika zaidi katika maeneo ya mijini na
ya uzalishaji. Maeneo hayo ni kama vile mashamba ya kikoloni, migodini na mahali
walipoishi watawala wa kikoloni.
Ubaguzi wa rangi ulijitokeza katika utoaji wa huduma za maji na umeme. Ubaguzi
huu ulidhihirika zaidi katika maeneo ya mijini. Huko huduma bora za maji na umeme
walipatiwa kwanza Wazungu, wakifuatiwa na Waasia na hatimaye Waafrika. Kutokana
na hali hii, baadhi ya maeneo ya miji mikubwa kama Dar es Salaam na Mwanza
yalijulikana kama Uzunguni na Uhindini. Maeneo ya mjini walipokaa Waafrika
wengi yaliitwa maeneo ya Uswahilini. Maeneo ya vijijini yalipatiwa huduma duni
zaidi ikilinganishwa na yale ya mijini, hali iliyosababisha watu wa vijijini kuhangaika
kutafuta huduma za maji na umeme. Maeneo ya vijijini yaliendelea kutumia kuni,
koroboi na taa za chemli kutoa mwanga wakati wa usiku.
Mchango wa ukoloni katika uhusiano wa Tanzania na mataifa yaliyoitawala
Kabla ya ujio wa wakoloni, jamii za Kitanzania zilikuwa na uhusiano wa kuheshimiana
na kushirikiana na jamii nyingine za Afrika na kwingineko. Uhusiano huu ulijengwa
kwa misingi ya biashara, ambapo jamii hizo zilibadilishana bidhaa kama vile dhahabu,
pembe za ndovu na vyakula. Ushirikiano huu ulizingatia maadili ya kutegemeana,
kusaidiana na kuaminiana. Biashara iliyofanyika kati ya jamii hizi ilichangia
kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Hali hii ya ushirikiano ilianza kubadilika baada ya ujio wa wakoloni kutoka Ulaya
Magharibi. Mataifa ya Ulaya, hususani Ujerumani na Uingereza, yalitawala maeneo
mbalimbali kwa lengo la kunyonya rasilimali za jamii za Kitanzania. Wakoloni
walivunja uhusiano wa asili uliokuwepo kwa kuanzisha mipaka mipya na kuleta
maadili ya kikoloni. Pia, waliweka sera mpya zilizovuruga maadili ya kijamii ya
Kitanzania, ambayo yalijengwa katika misingi ya utu, upendo, umoja, kusaidiana
na kuheshimiana kama jamii huru.
Baada ya ukoloni kushamiri, uhusiano kati ya jamii za Kitanzania na wakoloni uliingia
katika hali ya uhasama mkubwa. Mataifa ya kikoloni ya Ulaya Magharibi yalitumia
21
03/10/2024 18:15:09
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 21 03/10/2024 18:15:09
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 21

