Page 31 - Historia_Maadili
P. 31
Sura ya Pili Athari za ukoloni katika
maadili ya Kitanzania
FOR ONLINE READING ONLY
Utangulizi
Kuingia kwa ukoloni mwishoni mwa karne ya 19 kulisababisha kuanza
kupenya kwa maadili ya kikoloni, ambayo yaliidhoofisha mifumo asilia ya
maadili ya jamii za Kitanzania. Katika sura hii, utajifunza kuhusu dhana ya
maadili katika kipindi cha ukoloni na maadili ya jamii za Kitanzania wakati
wa kuingia kwa ukoloni. Vilevile, utajifunza athari za mfumo wa ukoloni
katika maadili ya Kitanzania na maadili ya Kitanzania yaliyodumishwa
katika kipindi cha ukoloni. Umahiri utakaoujenga utakuwezesha kuishi kwa
kuzingatia maadili ya Kitanzania.
Fikiri
Maadili ya sasa ya jamii za Kitanzania.
Dhana ya maadili wakati wa ukoloni
Dhana ya maadili wakati wa ukoloni inahusisha mifumo ya kiutawala, kisiasa,
kiuchumi na kiutamaduni ambayo ililetwa na wakoloni pamoja na ile iliyokuwepo
kabla ya ujio wa wakoloni katika jamii za Kitanzania. Kwa kiasi kikubwa, Waafrika
waliendelea kuziishi na kuzifuata mila na desturi zao, ingawa pia waliyapokea maadili
mapya kama vile imani za kiroho, mifumo ya kiutawala na tamaduni za kigeni. Kanuni
za kikoloni zilisisitiza uwajibikaji wa kila mtu, umiliki binafsi wa mali na heshima
kulingana na nafasi ya mtu katika jamii. Hata hivyo, kanuni hizi kwa kiasi kikubwa
zilikinzana na maadili ya Kitanzania yaliyokuwapo kabla ya ujio wa wakoloni.
Hii ni kwa sababu jamii nyingi ziliamini katika uwajibikaji wa pamoja, umiliki wa
mali kwa pamoja na heshima kwa wote bila kujali nafasi ya mtu katika jamii. Kwa
ujumla, maadili ya jamii za Kitanzania kabla ya ujio wa ukoloni katika jamii nyingi
yaliongozwa na mfumo wa usawa.
23
03/10/2024 18:15:09
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 23
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 23 03/10/2024 18:15:09

