Page 30 - Historia_Maadili
P. 30
mbinu za kijeshi na kisiasa kutawala jamii za Kitanzania. Hali hii ilileta migongano
ya mara kwa mara. Wazawa walilazimika kupigania na kulinda ardhi zao, utu na
uhuru wao dhidi ya utawala wa kigeni. Hali hii lilisababisha uadui kati ya wakoloni
na jamii mbalimbali za Kitanzania.
Ukoloni uliathiri kwa kiasi kikubwa uhusiano wa kijamii na kiuchumi wa jamii za
Kitanzania. Uhusiano wa kibiashara uliokuwa na mafanikio zamani sasa ulibadilika
FOR ONLINE READING ONLY
na kuwa wa kiunyonyaji. Wakoloni walipora rasilimali kama vile ardhi na madini
na kuwanyonya wafanyakazi wa Kitanzania katika mashamba na migodi yao.
Hii ilisababisha kuongezeka kwa umasikini na ukosefu wa haki miongoni mwa
Watanzania.
Mbali na uhasama, ukoloni pia ulileta athari kubwa kwenye utamaduni na mifumo
ya kijamii. Utamaduni wa kigeni ulienea katika jamii za Kitanzania na kudhoofisha
utamaduni na maadili ya asili. Hali hii ilichangia kuvunjika kwa mshikamano wa
kijamii na kuendeleza uhusiano hasi kati ya jamii za Kitanzania na wakoloni.
Ingawa ukoloni ulisababisha uhusiano mbaya baina yake na jamii za Kitanzania,
pia ulisababisha mwamko mpya wa utaifa wa kudai uhuru. Harakati za kudai uhuru
na kujikomboa zilichochea umoja miongoni mwa jamii za Kitanzania. Baada ya
Tanganyika kupata uhuru mwaka 1961, uhusiano mpya ulijengwa kati ya Tanganyika
huru na mataifa ya kigeni, yakiwemo mataifa yaliyokuwa yakiitawala. Uhusiano
huu ulijengwa katika misingi ya kimaadili iliyolenga kuimarisha umoja wa kitaifa,
kulinda uhuru, kujitegemea na kuheshimu haki za binadamu. Katika kipindi hicho
cha uhuru wa Tanganyika na mara baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar,
Tanzania ilijipambanua kama taifa lenye msimamo huru katika uhusiano wake na
mataifa mengine.
Zoezi la marudio
1. Eleza sababu za wakoloni kutoanzisha viwanda vya kuzalisha bidhaa katika
maeneo ya Tanzania wakati wa ukoloni.
2. Linganisha hali ya utoaji wa huduma za jamii wakati wa utawala wa
Wajerumani na Waingereza katika jamii za Kitanzania.
3. Fafanua namna ambavyo sera za utawala wa Wajerumani na Waingereza
zilivyokinzana na maadili ya jamii za Kitanzania.
4. Jamii za sasa za Tanzania zinaweza kujifunza nini kuhusu usimamizi wa
rasilimali na utawala kutoka kwa Wajerumani na Waingereza?
5. Kwa kurejelea utoaji wa huduma za kijamii wakati wa ukoloni, pendekeza
namna bora ya kuboresha utoaji wa huduma za kijamii katika Tanzania ya
sasa.
6. Tofautisha utoaji wa huduma za jamii wakati wa sasa na ule wa utawala wa
Wajerumani na Waingereza.
22
03/10/2024 18:15:09
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 22 03/10/2024 18:15:09
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 22

