Page 32 - Historia_Maadili
P. 32
Jamii za Kitanzania ziliundwa na makabila mbalimbali, kila moja likiwa na mila,
desturi, maadili na miundo ya kijamii ya kipekee. Hivyo, jamii hizi zilijikuta zikikinzana
na mifumo ya maadili ya kikoloni, ambayo ilikuwa na madhumuni ya kudhoofisha
mila na imani za wenyeji, kama vile imani za jadi, sherehe za kimila kama ndoa na
tohara na elimu ya jadi kama jando na unyago. Pia, taratibu na mienendo ya kimila
kama kuishi kijamaa, uwajibikaji, heshima na uongozi wa kijadi vilidhoofishwa.
FOR ONLINE READING ONLY
Ukoloni ulipoingia na kujiimarisha, uliingiza mifumo mipya ya kimaadili na kijamii,
ambayo mara nyingi ilikinzana na mila za wenyeji. Mifumo hiyo ya kikoloni ililenga
kuzidhoofisha mila na imani za kiasili, zikiwemo dini za jadi na mila na desturi zao.
Mtazamo wa kikoloni ulipuuzia vipengele vya kuishi kidugu katika jamii za wenyeji
na badala yake ulisisitiza ubinafsi na maadili mengine ya kikoloni ambayo yalikuwa
mapya kwa jamii za Kitanzania.
Kazi ya kufanya 2.1
Umealikwa kuwakilisha shule yako katika semina kuhusu mada isemayo Vijana
na Maadili. Andaa muhtasari utakaoutumia kuwasilisha mawazo yako kwa
kutumia dondoo zifuatazo:
(a) Umuhimu wa maadili katika jamii; na
(b) Nafasi ya vijana katika kuyaenzi na kuyaendeleza maadili katika jamii.
Maadili ya jamii za Kitanzania wakati ukoloni unaingia
Katika jamii za Kitanzania, misingi ya maadili ilijengwa juu ya umoja, ushirikiano
na mshikamano miongoni mwa wanajamii. Vilevile, utunzaji wa mazingira, heshima
kwa wazee na viongozi na utunzaji na ulezi wa familia na jamaa vilikuwa ni sehemu
muhimu ya maadili hayo. Aidha, nidhamu, uaminifu na utii kwa mila, miiko na
desturi za jamii zilikuwa nguzo kuu za maadili. Hata wakati wa ukoloni, misingi hii
iliendelea kudumishwa kwa kiasi kikubwa na jamii za Kitanzania licha ya changamoto
zilizokuwepo.
Ukoloni ulipoingia katika jamii za Kitanzania mwishoni mwa karne ya 19, mfumo
wa maadili uliokuwepo, ambao ulilenga kujenga mshikamano wa kijamii, kuheshimu
tamaduni na kuishi kwa amani na utulivu. Mfumo huu ulijikita katika mila na desturi
zilizorithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine, ukizingatia ushirikiano, utu, haki
na heshima. Ingawa kulikuwa na makabila mbalimbali Tanzania, mila na desturi za
makabila hayo zilifanana kwa kiasi kikubwa.
24
03/10/2024 18:15:09
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 24
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 24 03/10/2024 18:15:09

