Page 34 - Historia_Maadili
P. 34
Kadhalika, uvumilivu ulikuwa msingi muhimu wa maadili ya jamii za Kitanzania.
Watu walifundishwa umuhimu wa kuvumiliana na kuheshimu tofauti za watu wengine,
iwe ni za kikabila, kidini au kiutamaduni. Hivyo, mila na desturi zilikuwa na nafasi
kubwa katika kuyaunda maadili ya jamii. Sherehe za kijamii kama vile harusi, jando
na unyago, imani za kidini na mila zilitumika kama fursa za kujenga mshikamano
wa kijamii na kufundisha maadili kwa vizazi vipya.
FOR ONLINE READING ONLY
Dini za jadi: Wakati ukoloni ulipoingia, dini za jadi zilikuwa na nafasi muhimu katika
kuunda maadili ya jamii. Watu waliamini katika nguvu za asili, mizimu na miungu.
Imani hizi ziliathiri na kukuza imani za watu na jinsi watu walivyoheshimu mazingira,
walivyotekeleza shughuli za kilimo na walivyoishi kwa maelewano. Maadili ya dini
za jadi yalisisitiza ushirikiano, upendo, heshima, umoja kwa wanajamii, pamoja na
kudumisha, kukuza na kufuata mila na desturi zilizorithiwa kutoka kizazi kimoja
hadi kingine. Dini za jadi pia zilitumika kama njia mojawapo ya kusimamia maadili
katika jamii. Kwa mfano, waliokaidi miiko, maagizo na taratibu za jamii waliadhibiwa
kwa njia mbalimbali kama vile mizimu na wazee kwa utovu wa nidhamu. Vilevile,
matatizo mbalimbali katika jamii yalitatuliwa kwa njia za kiimani kupitia matambiko
na mbinu nyingine zilizohusiana na dini za jadi.
Utawala wa jadi: Wakati ukoloni ulipoingia, jamii za Kitanzania zilikuwa zikiongozwa
na mifumo ya jadi iliyotofautiana baina ya kabila moja na lingine. Mifumo hii
mara nyingi ilijikita katika kufanya uamuzi kijamii, ambapo majukumu ya uongozi
yalitekelezwa na machifu, wazee, au mabaraza ya wazee. Uamuzi wa viongozi hawa
uliheshimiwa na wanajamii wote kutokana na hekima na uwezo wao wa kudumisha
maelewano ndani ya jamii. Uongozi huo ulifanya uamuzi kwa faida ya jamii nzima
na si kwa masilahi ya watu wachache. Dhana ya utawala ilikuwa imefungamana kwa
karibu na utamaduni na maadili ya jamii, ikisisitiza uwajibikaji wa pamoja, heshima
na utii kwa mamlaka, uzalendo na ustawi wa jamii nzima.Vilevile, kila jamii ilikuwa
na mfumo wake wa utawala wa kijadi, unaoongozwa na machifu, wazee wa ukoo,
au viongozi wa kimila. Kwa mfano, katika jamii za Kitanzania kulikuwa na mifumo
thabiti iliyojengeka na kuwa na nguvu kubwa kama vile Nyarubanja, Ubugabire na
Umwinyi. Mifumo hii ya kiutawala ilijitokeza katika jamii kama Wahaya, Waha na
jamii za pwani mtawalia. Mifumo hii ilifungamanishwa mno na nguvu ya kiuchumi
hasa umiliki wa ardhi na ng’ombe. Pamoja na mambo mengine, viongozi katika jamii
hizi waliheshimiwa sana na walikuwa na jukumu la kuhakikisha haki, usalama na
mshikamano wa jamii iliyohusika.
Katika jamii ya Wanyamwezi mathalani kulikuwa na wasaidizi wa Mtemi walioitwa
Wanyampala. Mmoja wa wasaidizi wake aliitwa Mgawe aliyekuwa kiongozi wa
matambiko, Mtwale alikuwa kiongozi wa jeshi lililohakikisha usalama wa Utemi
26
03/10/2024 18:15:09
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 26 03/10/2024 18:15:09
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 26

