Page 39 - Historia_Maadili
P. 39
utoaji elimu katika kila jamii, ambapo elimu hiyo ilitolewa wakati wote na kwa
vitendo. Mafunzo ya jando na unyago yaliandaliwa kwa madhumuni ya kuwaandaa
vijana kwa maisha ya utu uzima na kuchukua majukumu ya kijamii. Mafunzo haya
yalitolewa kwa njia mbalimbali kama vile kilimo, ufugaji, uwindaji, mapishi, ujenzi
na uvuvi. Vilevile, elimu ilitolewa kupitia hadithi, methali na uzoefu wa vitendo.
FOR ONLINE READING ONLY
Hii iliwawezesha wanajamii, hususani watoto na vijana, kupata maarifa stahiki na
ujuzi muhimu.
Mamlaka za kikoloni zilianzisha mifumo rasmi ya elimu iliyofuata mfumo wa elimu
na maadili ya kimagharibi ya Ulaya. Shule za wamisionari zilifundisha masomo
yanayohusu maadili ya kwao, huku mara nyingi zikikataa na kupinga mila, tamaduni
na desturi za Kitanzania kuendelea kutumika miongoni mwa wanajamii. Kwa mfano,
wanafunzi mara nyingi waliadhibiwa kwa kuzungumza lugha zao za asili shuleni na
walisisitizwa kujifunza na kufuata desturi na maadili ya kimagharibi yaliyohifadhiwa
na wazungu kupitia mfumo wa ukoloni.
Hali kadhalika, mfumo wa elimu ya kikoloni ulisababisha mabadiliko makubwa
ya kiutamaduni. Watanzania wengi waliosoma shule hizi walifuata njia za kufikiri,
kuvaa na kuenenda Kizungu, ambazo zilipingana na mila, desturi na maadili ya
Kitanzania. Watumishi wa serikali ya kikoloni walilazimika kuvaa mavazi maalumu
kama sare kwa mfano maaskari na manesi. Watumishi wengine walivaa mavazi
yaliyoelekezwa na idara zilizohusika kama ya elimu, mahakama na wahudumu wa
ofisi. Hali hii ilijenga matabaka kati ya wasomi walioelimika, ambao walikuwa
wameshikamana zaidi na maadili ya kikoloni na wale ambao hawakupata elimu ya
kikoloni na waliodumisha njia za maisha za jadi. Kuwagawa Watanzania lilikuwa
moja ya malengo makuu ya wakoloni katika sera yao ya “wagawe ili uwatawale”.
Hivyo, hali hii ilichangia mmomonyoko wa kimaadili na kiutamaduni na hivyo
kusababisha kuenea na kukua kwa kanuni za kiutamaduni za kimagharibi na hivyo
kudunisha maadili ya Kitanzania.
Afya: Kabla ya ujio wa wakoloni, jamii za Kitanzania zilikuwa na mifumo mbalimbali
ya utoaji huduma za afya, kulingana na tamaduni na mila za jamii iliyohusika. Ingawa
hakukuwa na hospitali au vituo vya afya kama vilivyo sasa, hii haimaanishi kuwa
huduma za afya hazikuwepo. Kulikuwa na matumizi ya dawa za asili zilizotokana
na mimea na vifaa vingine kama vile mafuta au maji, ambazo zilitumika kutibu
magonjwa mbalimbali. Dawa hizi zilipatikana kwa urahisi katika mazingira yao.
Kulikuwa na wataalamu waliobobea katika masuala ya afya kama vile waganga
wa mitishamba, wakunga na ngariba waliokuwa na jukumu la kutibu na kuzuia
31
03/10/2024 18:15:10
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 31 03/10/2024 18:15:10
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 31

