Page 27 - Historia_Maadili
P. 27
zilizopewa kipaumbele ni zile zilizozalisha mazao ya biashara, hususani kahawa na
pamba, pamoja na vituo vya wamisionari. Kwa mfano, shule nyingi katika Tanganyika
zilijengwa katika maeneo ya Kilimanjaro na Bukoba.
Malengo ya elimu iliyotolewa na Waingereza yalikuwa kuwapatia wananchi maarifa
yatakayowasaidia kuendeleza mipango na mikakati ya kikoloni. Hii ilifanywa kwa
FOR ONLINE READING ONLY
kuwapa wananchi elimu ya mbinu bora za kilimo na ufugaji na elimu ya afya. Pia,
iliwaandaa mabwanyenye uchwara ambao walisaidia kuongoza na kufundisha utii
na unyenyekevu ili kutekeleza maagizo na maelekezo ya serikali ya kikoloni. Elimu
ilitolewa katika ngazi zifuatazo: elimu ya msingi (darasa la 1- 4), elimu ya kati
(darasa la 5-8) na elimu ya sekondari (darasa la 9-12). Mtaala wa elimu ulijikita
zaidi katika kufundisha mambo ya kigeni, hivyo maudhui yaliyofundishwa shuleni
hayakuwasaidia wananchi kutatua matatizo yao ya kila siku. Kwa mfano, wanafunzi
walifundishwa kuhusu mila, tamaduni na desturi za Kiingereza badala ya mila zao
za asili.
Kwa upande wa Zanzibar, Waingereza walitoa elimu iliyoendeleza matabaka ya
kijamii. Wazanzibari walifundishwa jinsi ya kuwa watiifu na waaminifu kwa Sultani
na viongozi wao, ambao wengi walikuwa Waarabu. Waarabu walipewa elimu maalumu
iliyowawezesha kuendelea kujiona kuwa bora kuliko Waafrika. Ubaguzi huu katika
utoaji wa elimu ulikuwa kikwazo kikubwa kwa Watanganyika na Wazanzibari.
Aidha, ubaguzi wa kikanda na kimaeneo ulikuwa dhahiri katika mfumo wa elimu,
ambapo shule nyingi zilijengwa katika maeneo ya uzalishaji mali kama Moshi,
Bukoba, Mbeya na Mwanza. Maeneo ya Rukwa na Kigoma yalikuwa na shule chache
kwa kuwa hayakuwa maeneo ya uzalishaji mali. Hivyo, wananchi wa maeneo haya
walinyimwa fursa za elimu. Wananchi hawa waliendelea kwenda kufanya kazi
za manamba katika mashamba na migodi ya kikoloni. Hivyo, elimu iliyotolewa
iliwafaidisha wachache pekee kwani hata shule zilikuwa chache na zilitoa elimu
kwa watoto wa machifu. Kwa mfano, Shule ya Wavulana Tabora ilikuwa maalumu
kwa watoto wa machifu.
Afya: Huduma za afya wakati wa utawala wa Waingereza zilitolewa kwa lengo la
kuziendeleza na kuzilinda afya za wananchi ili wawe na nguvu za kushiriki kikamilifu
katika shughuli za kuendeleza uchumi wa kikoloni. Pamoja na kwamba Waingereza
walihitaji nguvukazi yenye afya, bado huduma za afya zilikuwa chache na duni.
Sehemu zilizopata huduma za afya ni zile zilizo kwenye maeneo ya uzalishaji mali,
makazi ya walowezi na vituo vya wamisionari.
Kama ilivyokuwa katika elimu, huduma za afya pia zilitolewa kwa misingi ya ubaguzi
wa rangi. Huduma bora zaidi zilitolewa kwa Wazungu, wakifuatiwa na Waasia, huku
Waafrika wakipewa huduma za kiwango cha chini. Waingereza hawakuwaandaa
Waafrika kuwa matabibu wa ngazi za juu, bali walifundishwa kuwa matabibu wa
ngazi za chini. Vilevile, hospitali na vituo vya afya vilifuata misingi hiyo ya ubaguzi,
19
03/10/2024 18:15:08
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 19 03/10/2024 18:15:08
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 19

