Page 25 - Historia_Maadili
P. 25
Kazi ya kufanya 1.5
Shule yako imealikwa kushiriki mdahalo katika shule ya jirani; andaa hoja
utakazotumia katika mdahalo huo kuhusu mada inayosomeka, “Utawala
FOR ONLINE READING ONLY
wa Waingereza ulikuwa na manufaa makubwa ya kiuchumi katika jamii za
Tanganyika na Zanzibar.”
Mabadiliko ya kisiasa wakati wa utawala wa Waingereza
Baada ya Waingereza kukabidhiwa rasmi madaraka, serikali iliimarisha misingi
ya utawala kwa kuweka taratibu na sheria ili kurejesha hali ya utulivu iliyotoweka
wakati wa vita. Awali, Waingereza waliendelea kutumia mtindo wa utawala uliokuwa
ukitumiwa na Wajerumani. Hata hivyo, baadaye walibadilisha mfumo wa utawala
kwa kuanza kuwatumia viongozi wa jadi katika shughuli za utawala. Viongozi
hawa walikuwa na majukumu ya kusimamia maagizo ya serikali, kukusanya kodi,
kufanya sensa ya watu na mifugo, kuwa na daftari la walipa kodi na kuamua kesi
zilizofikishwa katika mahakama zao. Majukumu haya yalitekelezwa chini ya
usimamizi wa mabwana shauri wa Kiingereza waliokuwa na jukumu la kufafanua
sheria za kikoloni kwa wananchi.
Mtindo wa kisiasa wa kuwatumia machifu ulikuwa ni chombo cha kuendeleza
mipango ya ukoloni ya kuwakandamiza na kuwanyonya wananchi. Waingereza
walisisitiza sana ukabila katika mipango yao ili kuwagawa na kuwadhibiti wananchi.
Kwa mfano, kwenye mashamba na migodi, vibarua walipangiwa mabweni ya kulala
kwa misingi ya kikabila. Aidha, ubaguzi ulionekana katika shule na hata kwenye
mashindano ya ngoma na michezo ya jadi.
Ili kuimarisha utawala wa Waingereza, sheria na kanuni mbalimbali zilitungwa kwa
lengo la kuwakandamiza wananchi. Sheria zote hizi zililenga kuwanufaisha Wazungu
na Waasia. Wakoloni walitumia mbinu za kuwalaghai machifu kwa kuunda shirikisho
la machifu kwa kila kabila na kumteua chifu mmoja kuwa kiongozi mwandamizi wa
wengine. Kwa mfano, Marealle aliteuliwa kuongoza machifu wa Kichaga, Fundikira
aliteuliwa kuongoza machifu wa Kinyamwezi, Makwaia aliteuliwa kuongoza machifu
wa Kisukuma na Chifu Luther Kingu alichaguliwa kuongoza machifu wa Iramba.
Waingereza walitumia mtindo wa utawala uliokuwa ukijulikana kama utawala wa
kiuwakala ulioanzishwa na Gavana Sir Donald Cameron mwaka 1926. Mtindo
huu uliendeshwa kwa kutumia makamishna wa majimbo na wilaya. Makamishna
wa wilaya ndio waliokuwa kiungo kati ya serikali ya kikoloni na serikali za mitaa
zilizoongozwa na machifu wakisaidiwa na majumbe.
17
03/10/2024 18:15:08
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 17
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 17 03/10/2024 18:15:08

