Page 22 - Historia_Maadili
P. 22
Jamii zilivyoathirika na utawala wa Wajerumani
Wajerumani walijenga himaya yao ya kikoloni katika Afrika Mashariki ya Kijerumani
kuanzia mwaka 1885. Ili kufanikisha malengo yao ya kiuchumi, Wajerumani walianza
kutafuta njia mbalimbali za kiuchumi zilizoweza kuwaletea faida. Miongoni mwa
njia hizo, walitafuta maeneo mapya ya kibiashara, ambapo walijipenyeza katika
FOR ONLINE READING ONLY
maeneo ya bara kwa kufuata njia za biashara ya masafa marefu zilizotumiwa na
jamii za Kitanzania kabla ya ukoloni. Wakati huohuo, walijenga ngome za kijeshi na
vituo vikubwa huku wakiwabadilisha au kuwaondoa kwa nguvu watawala wa jadi
waliokuwepo. Walianzisha mfumo wa utawala uliokuwa chini ya liwali na maakida,
ambao aghalabu walikuwa Waarabu na watu kutoka sehemu nyingine za Afrika,
hususani Waswahili. Kwa ujumla, karibu jamii zote katika Afrika Mashariki ya
Kijerumani ziliathiriwa na utawala wa Wajerumani. Kwa mfano, baadhi ya jamii
zilizoathirika ni pamoja na Wanyamwezi, Wazigua, Wayao, Wangindo, Wamatumbi,
Wambunga, Wahehe, Wachaga, Wameru na Waha.
Jamii za Kitanzania zilizokuwa zimezoea kujitawala, zilivurugwa na kuja kwa utawala
wa Wajerumani. Wajerumani waliweka vibaraka waliotii sheria na matakwa yao.
Katika maeneo fulani au wilaya, walianzisha utawala wa kijeshi na kuondoa kabisa
utawala wa jadi, kama ilivyokuwa Iringa na Mahenge. Hivyo, wazawa walipoteza
nguvu yao ya kujitawala.
Wajerumani waliwataka wenyeji kulipa kodi, lakini wenyeji walikataa na hatimaye
machafuko na vita kadhaa vilizuka. Kwa mfano, mwaka 1898, kulizuka Vita ya
Maboga ambapo Wamatumbi walishindwa. Wamatumbi wa Kilwa na Wangindo wa
Liwale pia waliathirika kutokana na kulipwa ujira mdogo, kufanya kazi za sulubu,
kulipa kodi ya rupia tatu na kuadhibiwa vikali kwa makosa mbalimbali. Vilevile,
utawala wa Kijerumani ulisababisha kutothaminiwa kwa utu wa wanajamii wengi.
Wazazi au watu wazima walidhalilishwa mbele ya watoto wao, kwa mfano, kuchapwa
viboko pale waliposhindwa kulipa kodi ya kichwa au walipotenda makosa madogo
madogo.
Utawala wa Kijerumani ulisababisha utengano miongoni mwa jamii za Kitanzania.
Kwa mfano, Mangi Marealle wa Wachaga wa Marangu aliungana na Wajerumani
kumpiga Mangi Meli wa Moshi. Kwa ujumla, jamii za Kitanzania zilipata athari
katika uchumi na hata kisiasa, kwani mfumo wao wa kujitawala ulibadilishwa. Hali
hii iliwapa ujasiri wa kudai uhuru wao kwa njia na mbinu mbalimbali, ikiwemo vita.
14
03/10/2024 18:15:08
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 14 03/10/2024 18:15:08
HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI F2.indd 14

